
Wanadiplomasia watatu wa Qatar wamefariki na wengine wawili kujeruhiwa katika ajali ya gari karibu na kituo cha mapumziko cha Misri cha Sharm el-Sheikh, ambapo mkutano muhimu wa amani wa Gaza umepangwa kufanyika siku ya Jumatatu, Qatar imetangaza leo Jumapili. Nchi hii ya Kifalme ni mpatanishi mkuu katika vita kati ya Israel na Hamas.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Ubalozi wa Qatar mjini Cairo umeeleza “huzuni na masikitiko yake makubwa kufuatia vifo vya wanachama watatu wa utawala wake katika ajali mbaya ya barabarani huko Sharm el-Sheikh walipokuwa kwenye misheni.”
Miili ya wanadiplomasia hao itasafirishwa Doha leo Jumapili kwa ndege ya Qatar, kama vile majeruhi wawili wanaotibiwa hivi sasa Sharm el-Sheikh, ubalozi umesema katika taarifa.
Kwa mujibu wa Al-Qahera News, ambayo inahusishwa na idara za usalama za Misri, ajali hiyo ilisababishwa na dereva kupoteza udhibiti wakati wa akindesha gari.
Mazungumzo yamekuwa yakifanyika katika siku za hivi karibuni katika eneo la mapumziko la Bahari Nyekundu la Sharm el-Sheikh kwa lengo la kumaliza vita kati ya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Qatar, pamoja na Misri na Marekani, zilishiriki katika mazungumzo ya miezi kadhaa yaliyolenga kufikia mkubaliano katika ardhi ya Palestina, makubaliano ambayo yalifikia kilele cha usitishaji mapigano ulioanza siku ya Ijumaa.
Sharm el-Sheikh iliwapokea maafisa wa vuguvugu la Kiislamu la Palestina Hamas na Israel, pamoja na nchi wapatanishi, kwa mazungumzo makali wiki iliyopita yaliyolenga kupata mapatano hayo kwa kuzingatia mpango wenye vipengele 20 uliowasilishwa na Rais wa Marekani Donald Trump.
Mji huo utakuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele wa amani unaoanza siku ya Jumatatu, utakaoandaliwa na Donald Trump na Rais wa Misri Abdel Fattah Al Sisi, ambao utahudhuriwa na viongozi wa zaidi ya nchi 20, pamoja na Ufaransa na Uingereza.