Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdoğan, Rais wa Marekani Donald Trump, Rais wa Misri Abdel Fattah el-Sisi, na Emir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani wamesaini nchini Misri tamko la nia ya kumaliza vita vya Gaza, wakati wa Mkutano wa Amani wa Sharm el-Sheikh. Viongozi hao wamekubaliana kwamba amani ya Gaza lazima ijengwe juu ya misingi ya usawa na kuheshimiana.
“Tunasisitiza uvumilivu, heshima na fursa sawa kwa wote,” walisema viongozi hao katika azimio hilo lililosainiwa Jumatatu mjini Sharm el-Sheikh, Misri.
“Tunataka eneo hili liwe mahali ambapo kila mtu anaweza kufuatilia ndoto zake kwa amani, usalama na ustawi wa kiuchumi, bila kujali rangi, dini au kabila.”
Azimiio hilo liliongeza kuwa viongozi hao “wanalenga mtazamo wa kina wa amani, usalama na ustawi wa pamoja” unaojikita katika kuheshimiana na hisia ya umoja.
“Kwa roho hiyo, tunakaribisha maendeleo yaliyopatikana katika kuanzisha makubaliano ya amani ya kudumu na ya kina Gaza, pamoja na uhusiano wa kirafiki na wenye manufaa kwa pande zote kati ya Israel na majirani zake wa kikanda,” viongozi walisema katika azimio hilo.