Raia wa Cameroon walimiminika vituoni Jumapili kushiriki katika uchaguzi wa rais unaotarajiwa kumrejesha madarakani Paul Biya, mwenye umri wa miaka 92 na ambaye ndiye kiongozi mzee zaidi duniani anayehudumu kwa sasa. Hali ya upigaji kura ilielezewa kuwa tulivu, huku vituo vingi vya kura katika mji mkuu Yaoundé vikipokea idadi kubwa ya wapiga kura kabla ya kufungwa jioni.

Rais Biya, ambaye ameiongoza nchi hiyo tangu mwaka 1982, alikabiliwa na wagombea 11, wakiwemo Issa Tchiroma Bakary, waziri wa zamani wa ajira mwenye umri wa miaka 79, aliyevutia umati mkubwa wa vijana katika kampeni. Wataalamu wa siasa wanasema licha ya shauku ya mabadiliko, mfumo wa sasa wa kisiasa una uwezo mkubwa wa kuhakikisha matokeo yanampendelea Biya.

Kamerun Yaounde 2025 | Issa Tchiroma Bakary kama mgombea urais
Issa Tchiroma Bakary ameibuka kuwa mshindani mkuu wa BiyaPicha: Daniel Beloumou Olomo/AFP

Vijana wahamasika kwa matumaini ya mabadiliko

Kampeni za uchaguzi huu zimekuwa na mvuto zaidi kuliko chaguzi zilizopita, huku vijana wakiweka matumaini mapya ya mabadiliko kupitia sanduku la kura. Wengi wao wamekuwa wakilalamikia gharama kubwa za maisha, ukosefu wa ajira na huduma duni za kijamii, hali inayochochea kutoridhika na uongozi wa muda mrefu wa Biya.

Tume ya Uchaguzi imesema zaidi ya wachunguzi 55,000 wa ndani na kimataifa, wakiwemo wa Umoja wa Afrika, walisimamia uchaguzi huo. Matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa ifikapo Oktoba 26, huku baadhi ya majukwaa ya mtandaoni yakiahidi kuchapisha matokeo yao binafsi — hatua ambayo serikali imeikosoa kwa madai ya kujaribu kupotosha maoni ya umma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *