Afisa wa Urusi aliyeteuliwa kuiongoza Crimea amesema Jumatatu kwamba droni ya Ukraine imeshambulia ghala la mafuta katika mji wa Feodosia, mashariki mwa rasi hiyo, na kusababisha moto mkubwa. Shambulio hilo limeongeza mvutano unaoendelea kati ya Moscow na Kyiv, huku vita vikikosa dalili za kumalizika.
Kiongozi wa utawala wa Urusi katika eneo hilo, Sergei Aksyonov, alisema kupitia Telegram kwamba zaidi ya droni 20 zimedunguliwa na vikosi vya ulinzi wa anga, na hakuna majeruhi waliothibitishwa. Hata hivyo, hakutoa maelezo kuhusu ukubwa wa uharibifu uliosababishwa na shambulio hilo.
Ghala la mafuta la Feodosia na miundombinu mingine ya nishati na kijeshi ya Crimea imekuwa ikilengwa mara kwa mara na mashambulizi ya Ukraine tangu Urusi ilipoanza uvamizi wake mwaka 2022.
Wakati huo huo, Ukraine na Urusi zimezidisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati za kila upande, katika kipindi ambacho juhudi za kidiplomasia za kurejesha mazungumzo ya amani zimeendelea kukwama kwa miezi kadhaa.