
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekataa mwaliko uliotolewa kwa Tehran kwa ajili ya kushiriki katika Mkutano kuhusu Gaza uliopangwa kufanyika huko Sharm el Sheikh, Misri akisema kuwa hawezi kuketi pamoja na viongozi waliowashambulia wananchi wa Iran na wanaoendelea kuitishia nchi hii na kuiwekea vikwazo.
Sayyid Abbas Araqchi ametuma ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X akimshukuru Rais Abdel Fattah al Sisi wa Misri kwa mwaliko huo lakini akaweza wazi kwamba si Rais Masoud Pezeshkian wa Iran wala yeye mwenyewe ambao wangekutana na pande hizo hasimu.
Waziri wa Mambo ya Nje amebainisha haya akiashiria mashambulizi ya anga ya Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran wakati wa vita vya siku 12 vilivyoanzishwa na Israel dhidi ya nchi hiyo pamoja na vikwazo vya Magharibi vilivyokusudiwa kulenga sekta ya uchumi na nishati.
Araqchi amesema kuwa Iran inaunga mkono pakubwa uamuzi wowote mkabala wa Palestina kwa shabaha ya kuhitimisha mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.
“Iran inakaribisha mpango wowote wa kukomesha mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza ambao utahakikisha wanajeshi wa Israel wanaondoka katika eneo hilo ,Wapalestina wanahaki kamili ya kupata haki yao ya kimsingi ya kujitawala, na mataifa yote yanabeba dhima ya kuwajibika na kuwasaidia wananchi hao kufanikisha malengo yao halali.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa Iran inasalia kuwa nguvu muhimu katika kanda hii.
“Iran imekuwa, na itabaki kuwa nguvu muhimu kwa ajili ya amani katika eneo hili. Kinyume na utawala wa Israel unaofanya mauaji ya kimbari; Iran haina lengo la kuendesha vita bali siku zote inatilia mkazo kuhusu ushirikiano na amani,” amesema Abbas Araqchi.
Mkutano wa leo huko Sharm al-Sheikh uliopangwa kuongozwa na Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri na Donald Trump wa Marekani umeratbiwa ili kurasimisha usitishaji vita na kuandaa mikakati ya ujenzi na suala la uongozi baada ya vita vya mauaji ya kimbari ya miaka miwili ya Israel huko Gaza.
Nchi zaidi ya 20 zinatazamiwa kushiriki katika mkutano wa Sharm al Sheikh baada ya Israe na Hamas kufikia makubaliano.