
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Je, mabilionea wa teknolojia wanajiandaa na maangamizi ya akili mnemba (AI)?
-
- Author, Zoe Kleinman
- Nafasi, BBC
Inasemakana Mark Zuckerberg ameanza ujenzi katika eneo lake lenye ukubwa wa ekari 1,400 kwenye kisiwa cha Hawaii cha Kauai, kutoka mwaka 2014.
Anajenga makazi, yatakayo zalisha nishati na chakula. Maseremala na mafundi umeme wanaofanya kazi kwenye eneo hilo walipigwa marufuku kuzungumza juu ya ujenzi huo, kulingana na ripoti ya jarida la Wired.
Kuna ukuta wa futi sita unaozuia ili mradi usionekane.
Alipoulizwa mwaka jana ikiwa anatengeneza handaki la kujificha na maangamizi, mwanzilishi huyo wa Facebook alisema “hapana.” Eneo la chini ya ardhi lenye ukubwa wa futi za mraba 5,000 alielezea, “ni makazi na handaki.”
Pia amenunua makazi 11 katika kitongoji cha Crescent Park cha Palo Alto huko California, na kuweka nafasi ya chini ya ardhi ya futi za mraba 7,000.
Ingawa vibali vyake vya ujenzi vinasema ni vyumba tu vya chini ya ardhi, kulingana na New York Times, baadhi ya majirani wanasema anajenga nyumba kamili ya kujificha chini ya ardhi.
Kuna uvumi unaowazunguka matajiri wengine wa teknolojia, ambao baadhi wanaonekana kununua ardhi kwa wingi, kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za chini ya ardhi.
Reid Hoffman, mwanzilishi mwenza wa LinkedIn, anasema New Zealand ni eneo maarufu la ujenzi wa nyumba za aina hiyo za matajiri.
Je, wanajiandaa kwa vita, athari za mabadiliko ya tabia nchi, au tukio lingine baya ambalo sisi wengine bado hatulijui?

Tatizo ni nini?
Katika miaka michache iliyopita, maendeleo ya akili mnemba (AI) yameongeza na kuongeza orodha ya matatizo yanayoweza kutokea. Wengi wana wasiwasi juu ya kasi na ukubwa wa maendeleo hayo.
Ilya Sutskever, mwanasayansi na mwanzilishi mwenza wa Open AI, anaripotiwa kuwa mmoja wa wenye wasiwasi.
Kufikia katikati ya mwaka 2023, kampuni hiyo yenye makao yake mjini San Francisco ilizindua ChatGPT – ambayo sasa inatumiwa na mamilioni ya watu duniani kote.
Kufikia majira ya kiangazi, Bw Sutskever alikuwa anazidi kushawishika kuwa wanasayansi wa kompyuta wako kwenye ukingo wa kutengeneza akili jumla mnemba (AGI) – ambapo mashine zitakuwa na akili kama ya binadamu – kulingana na kitabu cha mwandishi wa habari Karen Hao.
Katika mkutano, Sutskever alipendekeza kwa wenzake kwamba wanapaswa kujenga makazi chini ya ardhi kwa ajili ya wanasayansi wakuu wa kampuni hiyo kabla ya teknolojia hiyo yenye nguvu haijatolewa.
“Kwa hakika tutajenga vyumba za chini ya ardhi kabla ya kuzinduliwa AGI,” inaelezwa kuwa alisema.
Wanasayansi wengi wa kompyuta na teknolojia, ambao baadhi yao wanafanya kazi kwa bidii kiukuza AI, pia wanaonekana kuogopa kile ambacho teknolojia hiyo itakifanya siku moja.
AGI inawezekana?

Chanzo cha picha, Getty Images
Wataalamu wakuu wa teknolojia wanadai kuwa AGI iko njiani inakuja. Bosi wa OpenAI Sam Altman alisema mwezi Desemba 2024 kwamba itakuja “mapema kuliko watu wengi ulimwenguni wanavyofikiria.”
Sir Demis Hassabis, mwanzilishi mwenza wa DeepMind, ametabiri itakuja katika miaka mitano hadi kumi ijayo.
Mwanzilishi wa Anthropic, Dario Amodei aliandika mwaka jana kwamba “AI yenye nguvu” inaweza kutokea mapema 2026.
Je, teknolojia hiyo inaweza kutekwa nyara na magaidi na kutumika kama silaha, au ikiwa itaamua yenyewe kwamba binaadamu ndio chanzo cha matatizo ya ulimwengu na kutuangamiza?
“Ikiwa teknolojia ina akili kuliko wewe, basi tunapaswa kuizuia,” ameonya Tim Berners Lee, muundaji wa Mtandao wa World Wide Web, akizungumza na BBC mapema mwezi huu.
“Lazima tuweze kuizima.”
Serikali zinachukua hatua za ulinzi. Huko Marekani, ambapo kampuni nyingi zinazoongoza za AI ziko, Rais Biden alipitisha agizo 2023 ambalo linataka kampuni kutoa matokeo ya majaribio juu ya usalama kwa serikali ya shirikisho – ingawa Rais Trump amebatilisha baadhi ya agizo hilo, akisema ni “kizuizi uvumbuzi.”
Wakati huo huo nchini Uingereza, Taasisi ya Usalama ya AI – shirika la utafiti linalofadhiliwa na serikali – lilianzishwa miaka miwili iliyopita ili kuelewa vyema hatari za AI.
Kuna haja ya kuogopa?

Vince Lynch, Mkurugenzi Mtendaji wa IV.AI yenye makao yake California, anasema kuna biashara zaidi kuliko uhalisia.
“Ni biashara nzuri,” anasema “Ikiwa wewe ni kampuni inayojenga kitu chenye akili zaidi ambacho hakijawahi kuwepo, watu watataka kukupa pesa.”
Alipoulizwa kama anaamini AGI itawahi kutokea, anavuta pumzi na kusema. “Kwa kweli sijui.”
Baadhi ya makampuni ya teknolojia yanasema hawajui ni kwa nini teknolojia zao hutoa jawabu namna zinavyotoa. Meta inasema kuna dalili kwamba mifumo yake ya AI inajiboresha.
Hata hivyo, haijalishi jinsi mashine zinavyokuwa na akili, kibayolojia ubongo wa mwanadamu una akili zaidi. Una takribani niuroni bilioni 86 na sinepsi trilioni 600, nyingi zaidi ya zile za akili mnemba.
Dame Wendy Hall, profesa wa sayansi ya kompyuta katika Chuo Kikuu cha Southampton, anasema “jumuiya ya wanasayansi inasema teknolojia ya AI ni ya kushangaza, lakini haiwezi kuifikia akili ya binadamu.”
Ubongo hauhitaji kuchukua muda katika kufanya jambo moja na jingine, na unabadilika kila mara ili kupata taarifa mpya.
Wataalamu wanasema, ukimwambia mwanadamu kwamba kuna viumbe wengine kwenye sayari ya mbali, mara moja watajifunza hilo, na litaathiri mtazamo wao kuhusu ulimwengu. Lakini kwa akili mnemba, italijua tu hilo ikiwa utaeendelea kulirudia.
AI pia hazina utambuzi wa ndani, ina maana kwamba hazijui kile wanachokijua. Wanadamu wanaonekana kuwa na uwezo wa kujichunguza, na wakati mwingine wana ufahamu, unaowaruhusu kujua wanachojua.
Ni sehemu ya msingi ya akili ya binadamu – ambayo bado haijafikiwa na akili ya maabara.