Bwana Guterres amepokea kwa faraja yake kubwa hatua hiyo ya kuachiliwa kwa mateka hao, miaka miwili tangu walipotekwa miongoni mwa takribani watu 250 wakati wa mashambulio ya kigaidi yaliyokuwa yaliyoongozwa na Hamas nchini Israeli tarehe 7 Oktoba 2023, akisisitiza juu ya mateso makubwa waliyoyapitia.
Kauli hiyo ya Katibu Mkuu ilitolewa wakati akielekea Sharm el-Sheikh, Misri, kuhudhuria mkutano wa amani kuhusu Gaza.
Mkutano huo wa kimataifa ulmetishwa baada ya majeshi ya Israeli kujiondoa katika baadhi ya maeneo ya Gaza, kwa mujibu wa makubaliano kati ya Israeli na Hamas yaliyosimamiwa na Marekani, Qatar na Uturuki.
Kupitia ujumbe kwenye mtandao wa X, Bwana Guterres alisisitiza tena wito wake wa kuachiliwa kwa miili ya mateka waliouawa na kuzitaka “pande zote kuzingatia mafanikio haya na kutimiza ahadi zao chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano ili kumaliza jinamizi huko Gaza.”

Vifaa vya matibabu vinapakuliwa kwenye ghala la WHO.
Tani 190,000 za misaada zimeidhinishwa kuingia Gaza
Wakati huohuo, mashirika ya Umoja wa Mataifa yameripoti maendeleo makubwa katika kupeleka misaada ya kibinadamu Gaza.
“Uboreshaji wetu wa shughuli za kibinadamu huko Gaza unaendelea vizuri,” limesema shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu Misaada ya Kibinadamu na Mmasuala ya Dharura OCHA, likieleza kuwa limepata idhini kutoka kwa Israeli kuruhusu tani 190,000 za chakula, vifaa vya kujenga makazi, dawa na misaada mingine kuingia Gaza ikiwa ni tani 20,000 zaidi ya makubaliano ya awali.
Kwa mara ya kwanza tangu mwezi Machi, gesi ya kupikia imeanza kuruhusiwa kuingia Gaza.
Aidha, “Mahema mapya kwa familia zilizofurushwa makwao, nyama iliyogandishwa, matunda mapya, unga na dawa pia zilivuka mpaka kuingia Gaza jana Jumapili,” imesema OCHA katika taarifa yake.
Jambo muhimu zaidi, shirika hilo limeripoti kwamba wafanyakazi wake na washirika wao sasa wanaweza kusafiri kwa urahisi zaidi “katika maeneo mengi” hatua iliyopokelewa vyema baada ya vikwazo vya mara kwa mara vya ufikiaji vilivyowekwa na mamlaka za Israeli.
Hii imewezesha timu za misaada kupeleka vifaa vya matibabu na dharura “katika maeneo yenye uhitaji mkubwa zaidi,” pamoja na kufanya tathmini za barabara kuhusu mabomu yaliyofichwa na kusaidia familia zilizo hatarini kutokana na mafuriko kabla ya msimu wa baridi.
“Huu ni mwanzo tu. Kama sehemu ya mpango wetu wa siku 60 za mwanzo za kusitishwa kwa mapigano, Umoja wa Mataifa na washirika wetu wataongeza wigo na kiwango cha shughuli zetu kufikisha misaada na huduma za kuokoa maisha kwa karibu kila mtu huko Gaza,” OCHA imeongeza.
Vipengele vikuu vya mpango wa kibinadamu
Mpango huo mpana unaoratibiwa na Mkuu wa Misaada ya Dharura wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher, unalenga kupanua huduma muhimu katika sekta za chakula, afya, maji, makazi na elimu:
- Misaada ya chakula: Kwa watu milioni 2.1 kupitia mgao wa chakula, msaada kwa majiko ya kuoka mikate, kurejesha ajira za wafugaji na wavuvi, pamoja na msaada wa kifedha kwa familia 200,000.
- Lishe bora: Uchunguzi wa lishe na utoaji wa chakula chenye virutubisho kwa watoto, vijana, na wanawake wajawazito au wanaonyonyesha.
- Huduma za afya: Kurejesha huduma za matibabu, dawa muhimu, ufuatiliaji wa magonjwa, huduma za dharura na uzazi, pamoja na afya ya akili na ukarabati.
- Maji na usafi wa mazingira: Kwa watu milioni 1.4 kupitia ukarabati wa mifumo ya maji, maji taka na taka ngumu, na usambazaji wa vifaa vya usafi.
- Makazi: Kutoa mahema, maturubai na vifaa vingine vya kujenga makazi kwa familia zilizo hatarini kabla ya baridi.
- Elimu: Kufungua tena maeneo ya muda ya kujifunzia kwa watoto 700,000 pamoja na vifaa vya shule na shughuli za kielimu.

Wapalestina wanarejea kwenye yale mabaki ya nyumba zao katika sehemu zilizoshambuliwa kwa mabomu katika Ukanda wa Gaza.
Athari za vita
Miaka miwili ya ghasia kubwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya Israeli yameziacha familia nyingi bila makazi ya kurejea.
Vurugu hizo pia zimezalisha mahitaji makubwa ya kimwili na kisaikolojia kote Gaza, ambayo mashirika ya Umoja wa Mataifa tayari yanafanyia kazi kuyashughulikia.
UNICEF, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, limesema kwamba “watoto wote milioni moja katika Ukanda wa Gaza wanahitaji msaada wa afya ya akili na kisaikolojia.”
Vita hivyo vimeharibu hisia za usalama, maendeleo na ustawi wa watoto, likiongeza kwamba wengi wao wanaonesha “dalili kali za msongo wa mawazo kama vile kujitenga, ndoto mbaya na kukojoa kitandani”.
Ili kuwasaidia watoto kupona na kushinda hofu zao, UNICEF inaendesha mpango wa kuwasaidia kisaikolojia ambapo waelimishaji huwafundisha watoto mbinu za kudhibiti msongo wa mawazo na kushughulikia mawazo au picha za machungu.
Kifaa kimojawapo kinachotumika ni “kitufe cha usalama” cha kufikirika ambacho watoto hubonyeza wanapohisi kuzidiwa na hali zao.
“Wakati wowote nilipohisi woga, ninaweka mkono wangu juu ya kitufe cha usalama na kuvuta pumzi ndani na nje. Ilinifanya nijisikie vizuri,” amesema Anas, mwenye umri wa miaka 15, mmoja wa watoto wanaonufaika na mpango huo.
Mwaka 2025, UNICEF iliripoti kuwa watoto 8 kati ya 10 wanaoshiriki katika mpango huo walionesha kupungua kwa dalili za msongo wa mawazo wa kiathari.