
Rais wa Marekani Donald Trump amewasili muda mfupi uliopita katika mji wa Sharm El Sheikh nchini Misri ambako atashiriki mkutano wa kilele utakaojadili mustakabali wa Gaza.
Kiongozi huyo wa Marekani anajaribu kutia msukumo wa kupatikana amani katika kanda ya Mashariki ya kati baada ya kuitembelea Israel.
Viongozi wakuu 19 wa nchi na serikali wanahudhuria mkutano huo wa Sharm El Sheikh utakaojumuisha pia hafla ya kusainiwa makubaliano ya amani ya kumaliza vita Gaza.
Miongoni mwa viongozi walioko Misri ni pamoja na rais Emmanuel Macron wa Ufaransa,Mahmoud Abbas wa mamlaka ya Wapalestina na Waziri mkuu Keir Starmer wa Uingereza pamoja na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na rais wa baraza la Ulaya Antonio Costa.
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz ambaye pia amekwenda Sharm El Sheikh amesema nchi yake itasimamia utekelezaji wa mpango huo wa amani.