Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania (INEC), imefanya marekebisho ya maeneo ya uchaguzi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Marekebisho hayo, ni pamoja na kufuta kata kumi, kutengua uteuzi wa wagombea saba wa udiwani, pamoja na kuhamisha vituo 292 vya kupigia kura vilivyokuwa kwenye kata zilizofutwa.

Katika taarifa yake kwa umma iliyotolewa Oktoba 12, 2025, na kutiwa saini na Mwenyekiti wa Tume, Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele, INEC imesema uamuzi huo umefikiwa baada ya tangazo la Serikali Namba 596 na Namba 600 la Oktoba 3, 2025, ambapo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) alitangaza marekebisho ya mipaka ya maeneo ya utawala na kufuta kata kadhaa.

Kwa mujibu wa INEC, kata zilizofutwa ni Litapunga, Kanoge, Katumba, Ilangu, Bulamata, Ipwaga, Mishamo, Ikolongo, Ndurumo, na Mtapenda zilizoko katika mikoa ya Katavi na Tabora.

Aidha, INEC imetengua uteuzi wa wagombea saba wa udiwani waliokuwa wameteuliwa katika kata hizo kabla ya kufutwa kwake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *