
Maafisa wa ngazi za juu wa Ukraine wameelekea Washington kwa ajili ya kushiriki mkutano pamoja na maafisa wa Marekani kuhusu ulinzi.
Hayo yameelezwa leo na ofisi ya rais Volodymyr Zelensky katika wakati ambapo Urusi imezidisha mashambulizi yake dhidi ya miundo mbinu ya nishati ya Ukraine huku Marekani ikipima uwezekano wa kuipelekea Ukraine makombora ya kisasa ya masafa marefu.
Timu ya maafisa wa Ukraine inayoongozwa na waziri mkuu Yulia Svyrydenko itajadili suala la kuimarishwa kwa mifumo ya ulinzi wa anga ya nchi hiyo pamoja na uwezo wake wa silaha, lakini pia mifumo yake ya nishati kabla ya kipindi cha baridi kali.
Wakati huohuo Urusi imesema hivi leo kwamba hakuna mpango wowote ulioandaliwa wa kufanyika mazungumzo kwa njia ya simu kati ya rais Vladmir Putin,na Donald Trump baada ya kiongozi huyo wa Marekani kuonya kwamba ataipelekea Ukraine makombora ya Tomahawk.