Benki ya Dunia (World Bank Group) imekuwa ikitambua kwa muda mrefu umuhimu wa utawala bora katika kuhakikisha matumizi ya fedha za umma yana tija. Dhamira hii ilipata msukumo mkubwa mwaka 1996 wakati Rais wa Benki hiyo wa wakati huo, marehemu Jim Wolfensohn, alipoonya kuhusu “Saratani ya Rushwa.” Leo hii, wataalamu na watunga sera wanazidi kusisitiza kuwa utekelezaji wa sera ni muhimu sawa na usanifu wake. Ili kuboresha utekelezaji, ni muhimu kutumia njia inayotegemea takwimu na viashiria sahihi vinavyoweza kufuatilia maendeleo, kubaini changamoto na kusaidia kufanya marekebisho kwa wakati.

Benki ya dunia imesema mpaka sasa, kumekuwa na mafanikio makubwa katika uchambuzi wa utawala bora kwa kutumia takwimu kupitia miradi mbalimbali.

Kadiri ukusanyaji wa takwimu ulivyokua, mtazamo umebadilika kutoka kuchukulia serikali kama taasisi moja kubwa hadi kuchunguza taasisi binafsi za umma zinazohusika moja kwa moja katika matumizi na utekelezaji wa sera kama vile wizara za afya, elimu na serikali za mitaa. Katika uchambuzi huu, imebainika kuwa uwajibikaji, uwazi na ufanisi wa utawala wa umma ni nguzo muhimu za mafanikio.

Utafiti

Ili kuendeleza mjadala huu na kugeuza mawazo kuwa vitendo, Idara ya Taasisi za Dunia (Institutions Global Department) ya Benki ya Dunia iliandaa Mkutano wa Taasisi za Umma kwa Maendeleo, uliowakutanisha watunga sera na watafiti, akiwemo Karthik Muralidharan, ambaye aliwasilisha ajenda ya mageuzi ya taasisi za sekta ya umma.

Muralidharan alisisitiza kuwa “kuboresha uwezo wa taasisi za umma katika kutoa huduma kwa wananchi kunaweza kutoa matokeo ya uwekezaji mara kumi zaidi kuliko kuongeza matumizi pekee.” Kauli hii ilitokana na tafiti alizofanya kuhusu watumishi wa umma na taasisi zinazohusika na utoaji wa elimu, ustawi wa wakulima, malezi ya utotoni na ajira vijijini nchini India.

Kuhusu maeneo ya kipaumbele kwa mageuzi, Muralidharan alibainisha mambo muhimu kwa serikali: “kutumia teknolojia na takwimu kuboresha ukusanyaji wa mapato; kupima takwimu kwa uhuru kwa ajili ya malengo na tathmini; kuweka muundo sahihi wa mishahara ya umma; na kuzingatia ushirikiano au mikataba na sekta binafsi pale sekta ya umma inapokuwa dhaifu.”

Maeneo haya ndiyo yanayopewa kipaumbele na wataalamu wa utawala na taasisi wa Benki ya Dunia katika kusaidia nchi wanachama. Miongoni mwa juhudi hizo ni kuunda viashiria vipya vya ukusanyaji taarifa kuhusu utawala bora, pamoja na taarifa za ndani za taasisi kuhusu matumizi ya fedha, idadi ya watumishi, na taratibu za kutathmini uwezo wa taasisi husika.

Utafiti ufanyike kwa ushirikiano

Lakini, ni taarifa gani hasa tunazohitaji kukusanya ili kusukuma ajenda hii mbele?

Mtaalamu Rema Hanna alisisitiza umuhimu wa kufanya tafiti kwa ushirikiano na taasisi za serikali. Alieleza kuwa tafiti nyingi za kitaaluma zimekuwa zikitegemea miradi midogo inayotekelezwa na mashirika yasiyo ya kiserikali, jambo linalopunguza uwezo wa kuelewa athari za sera kwa kiwango kikubwa.

Hanna amesema kuwa “Ushirikiano na taasisi za umma, unatoa fursa ya kujifunza zaidi kuhusu utekelezaji wa sera kwa pamoja, mwingiliano kati ya serikali na soko binafsi, na namna mazingira ya ndani yanavyoathiri matokeo ya sera.”

Wakati wa mkutano huo, wataalamu walitoa tafiti za kina kuhusu njia za kuboresha upangaji, uwazi na uwajibikaji wa taasisi za umma zinazohusika na udhibiti na ununuzi wa umma, wakionesha uwezo mkubwa wa mbinu hizi katika kuleta mageuzi halisi.

Kwa ujumla, matumizi ya umma duniani mara nyingi hayatoi matokeo yanayotarajiwa kutokana na udhaifu wa taasisi, motisha hafifu na uwajibikaji mdogo.– Hii naomba uiweke kama quote kubwa kwenye story

Hata hivyo, kwa kutumia takwimu mpya na utafiti wa kisasa, fursa ipo ya kuimarisha taasisi na hivyo kuboresha huduma kwa wananchi.

Kuimarisha uwezo wa taasisi za umma ni miongoni mwa mikakati madhubuti zaidi ya maendeleo na sasa Idara ya Taasisi za Dunia ya Benki ya Dunia inaendelea kukusanya takwimu na ushahidi muhimu ili kufanya hili liwezekane.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *