
Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni wa Israel ametangaza kuwa utawala huo dhalimu una mipango ya kuharibu mahandaki na njia za chini ya ardhi za Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas huko Ghaza baada ya kuachiliwa huru mateka wa Kizayuni.
Israel Katz amesema hayo kwenye taarifa yake ya jana Jumapili na kuongeza kuwa: “Changamoto kubwa ya Israel baada ya awamu ya kuachiliwa huru mateka itakuwa ni kuharibu mahandaki huko Ghaza.”
“Nimeamuru jeshi kujiandaa kutekeleza opresheni hiyo,” Katz alisema.
Baada ya kupita zaidi ya miaka miwili ya mashambulizi ya kigaidi na kikatili ya Israel na kuua shahidi makumi ya maelfu ya Wapalestina, utawala ghasibu wa Kizayuni umelazimika kusalimu amri mbele ya Muqawama wa Wapalestina na mashinikizo ya kimataifa na kuidhinisha utekelezaji wa makubaliano ya kusimamisha jinai zake za mauaji ya umati na kubadilishana mateka kati yake na makundi ya Muqawama wa Palestina.
Ofisi ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ilitangaza mapema Oktoba 10 kwamba baraza la mawaziri la utawala huo pandikizi limeidhinisha utekelezaji wa makubaliano ya kumaliza vita katika Ukanda wa Ghaza.
Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya siku nne za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya pande hizo mbili katika mji wa Sharm el-Sheikh nchini Misri yaliyohudhuriwa pia na wajumbe kutoka Uturuki, Misri na Qatar, chini ya usimamizi wa Marekani.
Chini ya makubaliano hayo, jeshi la Israel lilitakiwa kuondoka katika kile kinachoitwa “mstari wa njano” ndani ya saa 24, na baada ya hapo Hamas itawaachilia huru mateka waliobakia walio hai ndani ya saa 72.
Hadi hivi sasa karibu Wapalestina 67,682 wameshathibitishwa kuuawa shahidi na 170,033 kujeruhiwa, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wadogo, tangu jeshi la utawala wa Israel lilipoanzisha mauaji ya umati huko Ghaza, Oktoba 7, 2023.