
Mgao huo, uliotangazwa Jumatatu na Mratibu wa Misaada ya Dharura wa Umoja wa Mataifa Tom Fletcher, utaunga mkono ongezeko la haraka la shughuli za utoaji msaada katika Ukanda wa Gaza, ukijumuisha chakula, maji, huduma za afya na makazi kwa raia walioathiriwa na miaka miwili ya mzozo.
Hatua hiyo inafuatia mgao wa dola milioni 9 wiki iliyopita kwa ajili ya kuhakikisha upatikanaji wa mafuta kwa hospitali na huduma muhimu, na hivyo kufanya jumla ya fedha za hivi karibuni za CERF kwa Gaza kufikia dola milioni 20.
Tangazo hili limekuja wakati usitishwaji wa mapigano uliosimamiwa na Marekani, Qatar na Misri ukiendelea kudumishwa, sambamba na kuachiwa kwa mateka wa Kiyahudi na wafungwa wa Kipalestina, hali ambayo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameielezea kama “matumaini ya utulivu baada ya miezi ya uharibifu.”
Ongezeko la haraka la msaada linahitajika
Umoja wa Mataifa na washirika wake wanaongeza kasi ya operesheni zao kote Gaza kadri fursa za ufikiaji zinavyoboreka, wakifikisha msaada wa kuokoa maisha katika maeneo ambayo yalikuwa yamekatika kwa miezi kadhaa.
Hata hivyo, ongezeko kubwa la fedha linahitajika kutokana na wingi wa mahitaji.
Bwana Fletcher ameonya kuwa bila michango mipya kwa CERF, msaada muhimu hautaweza kuendelea kuwafikia wanaouhitaji.
Akizungumza kutoka Sharm el-Sheikh, Misri, kabla ya mkutano wa kilele kuhusu Gaza, amesema kuwa juhudi za kibinadamu za Umoja wa Mataifa zinaendelea katika kile alichoita “wakati wa matumaini tete kwa wengi.”
“Huu ni wakati wa fursa, lakini pia ni wakati unaohitaji uvumilivu wenye msimamo, ubunifu, na ukarimu endelevu,” amesema.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na misaada ya Dharura OCHA, timu za Umoja wa Mataifa sasa zimepata idhini ya Israel kuingiza tani 190,000 za msaada, huku gesi ya kupikia ikiingia Gaza kwa mara ya kwanza tangu Machi na chakula zaidi, mahema na vifaa vya tiba vikiendelea kuwasili kila siku.