China imesema iko tayari “kupambana hadi mwisho” katika vita vya kibiashara na Marekani, kufuatia tangazo la Rais Donald Trump kwamba ataweka ushuru wa ziada wa asilimia 100 kwa bidhaa zote kutoka China. Msemaji wa wizara ya biashara ya China alisema Jumanne kuwa msimamo wa nchi hiyo kuhusu vita vya ushuru unabaki uleule: “Mkitaka kupigana, tutapigana hadi mwisho; mkitaka mazungumzo, mlango uko wazi.” Kauli hiyo imeibua wasiwasi mpya kuhusu kuongezeka kwa mvutano kati ya uchumi mkubwa zaidi na wa pili kwa ukubwa duniani.
Tangazo la Trump lilitolewa Ijumaa, likitaja hatua hiyo kama majibu kwa uamuzi wa Beijing kuweka vikwazo vipya vya usafirishaji wa madini adimu — sekta muhimu duniani inayotawaliwa na China. Hatua hiyo imeutikisa ulimwengu wa biashara, huku wachambuzi wakionya kuwa vita vya kibiashara vinaweza kuathiri vibaya masoko ya hisa na mahusiano ya kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.
Je, nani anaweza kushinda vita vya biashara?
Trump pia alisema Marekani itaanza kuwekea vikwazo vya usafirishaji wa programu muhimu za kiteknolojia kuanzia Novemba Mosi, akidai kuwa Beijing inatumia teknolojia hizo kwa faida ya kijeshi. Hatua hiyo imezidisha hofu kuhusu usalama wa kidigitali na ushindani wa kiteknolojia kati ya Washington na Beijing, hasa katika sekta za akili bandia na chipu za kisasa.
Kwa upande wake, msemaji wa wizara ya biashara ya China alisisitiza kuwa hatua za udhibiti wa mauzo ya nje ni halali na zinatekelezwa kwa mujibu wa sheria za ndani na kanuni za kimataifa. Aliongeza kuwa China, kama “mkoa mkubwa wenye uwajibikaji,” itaendelea kulinda usalama wake wa kitaifa na pia usalama wa pamoja wa kimataifa, akisisitiza kuwa Beijing haijafunga milango ya mazungumzo ya kibiashara.