
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imesema kuwa bado ina msimamo wake ule ule wa kuhakikisha mateka wote wa Palestina walioko kwenye makucha ya utawala wa Kizayuni wanaachiliwa huru kutoka kwenye jela za kutisha za Israel.
Suala la kuendelea kukomboa mateka wa Palestina litaendelea kuwa moja ya vipaumbele vyetu vikuu hadi mateka wa mwisho aachiliwe kutoka kwenye jela za Wanazi wapya na kukombolewa maeneo yote ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni ikiwemo Quds Tukufu,” imesema sehemu nyingine ya taarifa ya HAMAS iliyotolewa jana Jumatatu.
Siku ya Ijumaa, makubaliano ya kusitisha mapigano yalifikiwa kati ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS, na hivyo kukomesha miaka miwili ya jinai na mashambulizi ya kigaidi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Ukanda wa Ghaza.
Awamu ya kwanza ya makubaliano hayo, iliyosimamiwa na Misri na Qatar kwa jina la “mpango wa pointi 20” uliopendekezwa na rais wa Marekani Donald Trump, itajumuisha kubadilishana mateka wa Israel wasiopungua 50 walioko mikononi mwa Hamas katika mkabala wa kuachiliwa huru karibu mateka 2,000 wa Palestina kutoka katika makucha thakili ya Wazayuni maghasibu.
Zoezi la utekelezaji wa makubaliano hayo linaendelea ambapo miongoni mwa mateka wa Palestina wanaotarajiwa kuachiliwa huru ni 250 waliokuwa wanaotumikia kifungo cha maisha au cha muda mrefu, pamoja na wengine 1,718 waliotekwa nyara na jeshi la Israel huko Ghaza wakati wa mauaji ya umati ya miaka miwili yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni kwenye ukanda huo.