
Utawala wa Kizayuni mara kwa mara umekuwa ukipiga ngoma ya kuwapokonya silaha wananchi wa Ghaza na hilo imelifanya zaidi wakati wa vita vyake vya miaka miwili dhidi ya Ghaza, lakini hatimaye umelazimika kusalimu amri mbele ya Muqawama na mbele ya silaha za Wapalestina. Umekubali kusimamisha vita hivyo ili kubadilishana mateka, baada ya kushindwa kuwakomboa mateka hao kwa njia za kijeshi.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, Abdullah Al-Danan, mmoja wa viongozi wa chama cha Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Palestina alisisitiza jana Jumatatu kuwa, silaha ni mstari mwekundu kwa harakati za Palestina na kwamba harakati hizo haziko tayari kabisa kufanya mazungumzo juu ya suala hilo.
Al-Danan pia amesema: Israel, ambayo ina vifaru na ndege za kivita na inazitumia kufanya mauaji ya umati ndiyo inayopaswa kukabidhi silaha zake, si Wapalestina ambao wamelazimika kubeba bunduki kwa ajili ya kujihami na ukatili wa Israel.
Kuhusiana na makubaliano ya kubadilishana mateka na kusitisha vita Ghaza, al Danan amesema kuwa, Muqawama wa Palestina umeonesha unyumbulifu mkubwa kwenye makubaliano hayo kwani unajali sana roho na maisha ya Wapalestina wakiwemo wa Ukanda wa Ghaza.
Kabla ya hapo HAMAS nayo ilisema hivi karibuni kwamba, suala la kupokonywa silaha makundi ya Muqawama ya Palestina haliko kwenye meza ya mazungumzo ya kumalizwa vita vya Ghaza.
Vilevile Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imesema kuwa bado ina msimamo wake ule ule wa kuhakikisha mateka wote wa Palestina walioko kwenye makucha ya utawala wa Kizayuni wanaachiliwa huru kutoka kwenye jela za kutisha za Israel.
Jana mamia ya mateka wa Kipalestina walikombolewa kutoka jela za Israel kwenye awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano Ghaza.