
Dar es Salaam. Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Makamu Mwenyekiti (Bara), John Heche na Katibu Mkuu, John Mnyika pamoja na makada wengine watano na boadi ya wadhamini, wameitwa mahakamani kutokana na kukabiliwa na shauri la madai ya kuidharau mahakama.
Shauri hilo la madai mchanganyiko namba 25480 la mwaka 2025, linatokana na kesi ya inayoikabili Chadema hicho kuhusu mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali za chama baina ya Bara na Zanzibar, inayosikilizwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam.
Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 ilifunguliwa na Said Issa Mohamed, ambaye ni Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema (Zanzibar) na wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.
Walalamikiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga ni Bodi ya Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.
Wakati kesi hiyo ikiwa bado haijaanza kusikilizwa madai ya msingi, walalamikaji wamefungua shauri la madai dhidi viongozi hao wa Chadema, Heche, Mnyika na wenzao watano wakiwataka wajieleze ni kwa nini wasifungwe kama wafungwa wa madai, kwa kudharau amri ya mahakama hiyo.
Mbali ya Heche ambaye ni mjibu maombi wa kwanza, wengine ni Mnyika, Rose Mayemba, Brenda Rupia, Hilda Newton, Twaha Mwaipaya na Gervas Lyenda. Katika maombi hayo wamo pia wadhamini wa Chadema.
Kwa pamoja wanadaiwa kuidharau mahakama kwa kukiuka amri iliyoitoa ya zuio dhidi ya wadaiwa katika kesi ya msingi ya kikatiba, kutokufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali za chama mpaka kesi hiyo itakapomalizika.
Kutokana na shauri hilo wajibu maombi wametakiwa kufika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, Oktoba 15, 2025, saa 3:00 asubuhi kwa ajili ya kuhudhuria na kusikiliza maelezo ya mahakama kuhusu shauri hilo, lililopangwa kusikilizwa na Jaji Awamu Mbagwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya kutajwa kwa shauri hilo kwenda kwa wadaawa, ambayo Mwananchi limeiona, Heche, Mnyika na wenzao watakiwa kuwasilisha nyaraka ambazo wanakusudia kuzitumia katika utetezi wao katika shauri hilo.
“Fahamu kuwa kesi tajwa hapo juu imepangwa kwa ajili ya kutajwa Oktoba 15, 2025 saa 3:00, mbele ya Jaji A. Mbagwa,” inasomeka taarifa hiyo iliyosainiwa na Naibu Msajili na kuongeza:
“Unatakiwa kufika mahakamani bila kukosa na unatakiwa siku hiyo kutoa nyaraka zako unazokusudia kuzitimia katika kesi yako.”
Awali, waombaji na walalamikaji katika kesi ya msingi walifungua shauri dogo la maombi ya zuio la muda dhidi ya wadaiwa, wakiiomba mahakama itoe amri ya kuwazuia kufanya shughuli zozote za kisiasa na kutumia mali za chama mpaka kesi hiyo ya msingi itakapoamuliwa.
Juni 10, 2025 mahakama katika uamuzi iliyoutoa ilikubali hoja za walalamikaji ikatoa amri za zuio hilo kama walivyoomba.
Hata hivyo, waombaji katika shauri la kukiuka amri ya mahakama wanadai wajibu maombi wamekuwa wakikiuka amri hiyo.
Shauri hilo limefunguliwa chini ya hati ya dharura inayothibitishwa na mmoja wa mawakili wa waombaji, Mulamuzi Byabusha.
Katika hati ya maombi ya dharura, Byabusha anadai kati ya Juni 10 na Septemba 2025, wajibu maombi wamekuwa wakikaidi waziwazi na mara kwa mara amri hiyo halali.
Anadai wamekuwa wakiendesha na kushiriki shughuli mbalimbali za kisiasa, ikiwamo mikutano ya ndani ya Chadema, mikutano na wanahabari na hotuba kwa umma juu ya masuala ya kisiasa.
Pia anadai katika nyakati tofauti, wamewahamasisha viongozi wengine, mawakala na wanachama wa Chadema kuendelea kufanya shughuli mbalimbali za kisiasa za chama, kinyume cha amri halali ya mahakama.
Katika kiapo cha pamoja cha waombaji/walalamikaji wamebainisha tarehe mbalimbali ambazo wajibu maombi hao mmojammoja au kwa pamoja wamekuwa wakifanya shughuli hizo za kisiasa.
Hivyo, wanaiomba mahakama iamuru mjibu maombi wa kwanza mpaka wa saba wakamatwe na kuwekwa kizuizini kama wafungwa wa madai kwa kukaidi kwa makusudi amri halali ya mahakama.
Kuhusu kesi ya rasilimali
Chanzo cha hayo yote ni kesi ya msingi walalamikaji, ambapo wanadai kumekuwa na mgawanyo wa rasilimali usio sawa baina ya Bara na Zanzibar na ubaguzi katika masuala mbalimbali.
Kutokana na hayo, wanaiomba mahakama itamke kuwa wadaiwa wamekiuka kifungu cha 6A (1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019 na iwaelekeze wazingatie kifungu hicho.
Vilevile, wanaiomba mahakama itamke kwamba ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Zanzibar unaofanywa na wadaiwa ni kinyume cha sheria na ni batili.
Pia wanaomba mahakama isitishe kwa muda shughuli zote za kisiasa mpaka maagizo ya mahakama yatakapotekelezwa na zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi walalamikiwa watakapotekeleza matakwa ya sheria husika na gharama za kesi.
Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Oktoba 30, 2025 kuhusu pingamizi lililowekwa na walalamikiwa kuhusu mamlaka ya mahakama kwa kesi hiyo yenye madai ya kikatiba, kusikilizwa na Jaji mmoja badala ya jopo la majaji.
Awali, wadaawa waliwasilisha pingamizi la kumtaka jaji ajitoe, lakini liligonga mwamba, akisema hoja zao hazikuwa za msingi.