
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imejibu matamshi ya kibazazi ya Trump dhidi ya Tehran wakati alipolihutubia Bunge la Israel Knesset na imesema kuwa, Marekani ndiye nchi mzalishaji mkubwa wa ugaidi duniani na muungaji mkono mkuu wa wa utawala wa kigaidi umaofanya mauaji ya umati huko Ghaza, vipi inajipa mamlaka ya kimaadili ya kuwatuhumu watu wengine? Taarifa hiyo imesema kamwe wananchi wa Iran hawatasamehe wala kusahau jinai ya kinyama ya Marekani dhidi yao.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetolewa leo Jumanne Oktoba 14 kufuatia matamshi ya kibazazi ya rais wa Marekani dhidi ya taifa la Iran na kusema kuwa, katika hotuba yake kwenye bunge la Israel sambamba na kuashiria uvamizi wa Marekani kwenye vituo vya nyuklia ya Iran na maeneo yake ya ulinzi amedai kuwa eti litakuwa ni jambo zuri sana kama Marekani itaweza kufikia makubaliano ya amani na Iran.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalaani vikali tuhuma zisizo na msingi na madai ya kutowajibika na ya aibu yaliyotolewa na rais wa Marekani kuhusu Iran.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa: Marekani ambayo ni mzalishaji mkubwa wa ugaidi duniani na muungaji mkono wa utawala wa kigaidi wa Israel, haina haki wala mamlaka ya kimaadili ya kuwatuhumu wengine. Wananchi wa Iran ni taifa lenye heshima kubwa na shujaa na kamwe hawatosahau jinai za Marekani dhidi yao.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran vilevile imesisitiza katika taarifa yake hiyo ya leo Jumanne kwamba, kurudiwa madai ya uwongo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, hakuwezi kuhalalisha kwa vyovyote vile uvamizi wa Marekani na tawala za Kizayuni nchini Iran na kufanya mauaji dhidi ya watu muhimu na wapenda wa taifa hili.