Waziri wa habari wa Pakistan, amezungumzia mzozo wa mpaka wa nchi yake na Afghanistan, akidai kuwa operesheni hiyo ilifanywa kwa uratibu na India na kwamba shambulio hilo lilikuwa sehemu ya operesheni ya India inayojulikana kwa jina la Sindoor.

Waziri wa Habari wa Pakistan, Attallah Tarr amesema hayo kwenye mahojiano na Dunya TV na kuongeza kwamba mapigano ya umwagaji damu kati ya Afghanistan na Pakistan yamefanyika baada ya Afghanistan kuzungumza kwanza na India.

Pia amesema India haijatangaza kuwa operesheni Sindoor imeshamalizika, akiwa na maana ya shambulio la India dhidi ya Pakistan la mwezi Mei na kuongeza kuwa, serikali ya Taliban nchini Afghanistan ni sehemu ya operesheni hiyo ya India.

Waziri wa habari wa Pakistan pia amedai kuwa serikali ya Taliban haiwawakilishi kabisa watu wa Afghanistan bali ni sehemu ya operesheni ya Sindoor ya India dhidi ya Pakistan. Amesema kuwa Taliban wameshindwa kabisa kuchunga haki za wanawake, elimu na kutoa huduma za msingi kwa wananchi wa Afghanistan. Ndio maana hadi hivi sasa wananchi wa Afghanistan hawako pamoja nao.

Waziri wa habari za Pakistan aidha amesema: “Ikiwa ardhi ya Afghanistan itatumiwa vibaya dhidi ya Pakistan na wao (Taliban) wataendelea kuruhusu vigenge vya kigaidi kutumia eneo hilo kushambulia Pakistan basi tutaingia ndani ya ardhi ya Afghanistan na kuwashambulia magaidi hao.”

Waziri huyo wa Pakistan amesisitiza kwamba milango ya mazungumzo na Taliban bado iko wazi, lakini wakati huu mazungumzo yoyote yale yatakuwa na masharti mapya ya Pakistan. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *