
Jeshi la Israel limewauwa shahidi takriban Wapalestina sita huko Ukanda wa Gaza ndani ya saa 24, licha ya Tel Aviv hivi karibuni kufikia makubalianokuhusu utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mpango wa kusitisha vita.
Maafisa wa afya wa Palestina wameripoti Wapalestian hao wameuawa shahidi leo asubuhi wakati jeshi la Israel lilipoushambulia mji wa Gaza na maeneo ya kusini ya ukanda huo wa pwani. Israel imetekeleza mauaji haya dhidi ya Wapalestina ya kufikia makubaliano ya kusimamisha vita kati yake na harakati ya Hamas.
Wapalestina 5 wameuawa leo katika kitongoji cha Shuja’iyya baada ya jeshi la Israel kudai kuwa Wapalestina hao walivuka kile walichotaja kuwa “Mstari wa Njano” eneo ambalo Israel imetangaza kuondoka kama sehemu ya usitishaji vita.
Jeshi la Israel limewauwa shahidi raia hao wa Palestina wakati wakikagua nyumba zao.
Afisa wa afya wa Palestina ameeleza kuwa Mpalestina mwingine ameuliwa shahidi na wanajeshi wa Israel karibu na mji wa al-Fukhari mashariki mwa Khan Yunis wakati wanajeshi wa Israel walipolishambulia kundi la vijana wa Kipalestina.
Mapema mwezi huu, utawala wa Israel na harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) zilikubaliana kutekeleza awamu ya kwanza ya mpango ya kusitisha vita Gaza; mpango ambao unatarajiwa kuhitimisha vita vya mauaji ya kimbari vya zaidi ya miaka miwili yaliyoanzishwa na Israel dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza.
Wapalestina 68,000 wengi wao wakiwa wanawake na watoto wameuliwa shahidi katika mauaji ya kimbari ya Israel na washirika wake dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza.
Hazim Qassim Msemaji wa Hamas amelaani hujuma kubwa ya leo ya Israel dhidi ya Gaza na kuzitaka pande zote kufuatilia hatua za Israel na kuhakikisha kuwa utawala huo haukwepi wajibu wake kwa mujibu wa makubaliano ya kusimamisha vita Ukanda wa Gaza.