
Jeshi la Sudan (SAF) limetoa taarifa na kudai kuwa, zaidi ya wapiganaji 100 wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) wameuawa katika mapigano ya El Fasher, makao makuu ya Jimbo la Darfur Kaskazini huko magharibi mwa Sudan.
Katika taarifa yake, Divisheni ya 6 ya Kikosi cha Kutembea kwa Miguu cha Jeshi la Sudan ilitangaza jana kuwa, imefanikiwa kuzima shambulio kali lililoanzishwa na wanamgambo wa RSF kwenye mji wa El Fasher siku ya Jumapili.
Sehemu moja ya taarifa ya jeshi la Sudan imesema: “Vikosi vyetu vilipambana kwa ujasiri na washambuliaji na kuwasababishia hasara kubwa wavamizi hao vikiwepo vifaa vya kijeshi na kuua zaidi ya wapiganaji 100 na wengine kujeruhiwa.”
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, RSF ilianzisha mashambulizi hayo dhidi ya wanajeshi wa kutembea kwa miguu wa jeshi la Sudan SAF kwa kutumia magari ya kivita na vifaru viwili vikisaidiwa na mashambulizi ya silaha nzito.
Siku ya Jumamosi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ilidai pia kwamba mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za RSF yaliua raia 57 katika makazi ya muda ya wakimbizi wa ndani huko El Fasher. Hata hivyo, siku iliyofuata yaani siku ya Jumapili RSF ilikanusha vikali kuhusika na shambulio hilo.
Katika taarifa yake, msemaji wa RSF Al-Fateh Qurashi alisema, “Tunakanusha kabisa madai ya uongo yanayodai kuwa droni zetu zimeua raia kwenye makazi ya muda wa wakimbizi wa ndani huko El Fasher.”
Naye Denise Brown, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, amelaani kwa maneno makali zaidi mashambulizi ya mara kwa mara na ya makusudi yanayowalenga raia wasio na ulinzi huko Darfur Kaskazini.