
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Jihadul Islami ya Palestina imepongeza kuachiliwa huru mateka wa Palestina katika jela za kuogofya za kutokana na ushujaa wa wamamapambano wa kambi ya Muqawama na nguvu za mshikamano na umoja wa kitaifa wa Wapalestina.
Katibu Mkuu wa Jihadul Islami ya Palestina Ziyad al-Nakhalah alitoa kauli hiyo jana Jumatatu, kufuatia Israel kuwaachilia huru Wapalestina karibu 2,000 chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Marekani na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS.
“Kilichopatikana leo yaani kukombolewa idadi kubwa ya mateka wa Muqawama na wananchi wa Palestina, kisingeliwezekana bila wananchi na Muqawama kuwa kitu kimoja, bila ya ushujaa wa wanamapambano wa Palestina kwenye medani za mapambano kwa mshikamano na uungaji mkono wa dhati wa wananchi.
Mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yaliyofanyika nchini Misri kati ya Israel na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS yamepelekea kupatikana makubaliano ya kusimamisha vita Ghaza, kuondoka wanajeshi vamizi wa utawala wa Kizayuni kwenye ukanda huo na kubadilishana mateka.
Chini ya awamu ya kwanza ya makubaliano hayo, ambayo yalianza kutekelezwa saa sita mchana kwa saa za huko siku ya Ijumaa, Hamas iliwaachilia huru mateka 20 wa Israel wakiwa hai, huku mipango ikiendelea ya kuhamisha miili ya mateka wengine 28 waliouawa wakati wa mauaji ya umati yaliyofanywa kwa muda wa miaka miwili na utawala wa Kizayuni.
Kwa upande wake, Israel imewaachilia huru karibu Wapalestina 2,000, ambao walikuwa wanazuiliwa kinyume cha sheria kwenye jela za kutisha za Israel.
Miongoni mwao ni Wapalestina 1,700 waliokuwa wakishikiliwa na Israel bila kufunguliwa mashtaka tangu utawala huo ulipoanzisha mauaji ya umati huko Ghaza Oktoba 7, 2023. Mateka wengine 250 walikuwa wakitumikia kifungo cha maisha au kifungo cha muda mrefu.