Issa Tchiroma Bakary kiongozi wa upinzani nchini Cameroon ametangaza kwa upande mmoja kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais wa juzi Jumapili akimbwaga mshindani wake mkuu Rais Paul Biya ambaye amekuwa madarakani Cameroon kwa miaka 43. 

Tchiroma amebainisha haya mepama leo katika hotuba yake ya takriban dakika tano iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii. Ingawa vyombo rasmi vya habari havijatangaza matokeo ya uchaguzi wa rais wa Cameroon lakini, Issa Tchiroma Bakary amemtaka Paul Biya akubali ushindi wake huu. 

Amesema, wananchi wamechagua, na chaguo lao ni lazima liheshimiwe. 

Serikali ya Cameroon mapema wiki hii ilitahadharisha kuwa matokeo yanayotangazwa na Baraza la Katiba tu ndiyo yanayoweza kuhesabiwa kuwa matokeo rasmi. Baraza hilo la Katiba la Cameroon lina muda wa wiki mbili kutangaza matokeo ya uchaguzi. 

Issa Tchiroma Bakary Msemaji wa zamani wa serikali ya Cameroon na aliyekuwa mshirika wa Rais Biya kwa miaka 20 alikuwa mshindani mkuu wa Biya katika uchaguzi wa juzi wa rais. 

Mikutano ya kampeni ya kiongozi huyo wa upinzani ilikuwa ikivutia watu wengi sambamba na kuungwa mkono na muungano wa upinzani na jumuiya za kiraia.

Serikali ya Cameroon hadi sasa haijatoa taarifa yoyote rasmi kuhusu kauli ya kiongozi wa upinzani ya kujitangaza mshindi wa kiti cha urais. 

Paul Atanga Nji Waziri wa Utawala wa Majimbo wa Cameroon  hivi karibuni alionya kuwa Baraza la Katiba pekee ndilo lenye mamlaka ya kumtangaza mshindi, na kwamba tangazo lolote la upande mmoja la matokeo ya uchaguzi litahesabiwa kuwa “uhaini mkubwa”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *