fg

Chanzo cha picha, Reuters

    • Author, Tom Bennett
    • Nafasi, BBC

Jeshi la Israel linasema kundi la Hamas limewaachia mateka wote walioko Gaza ili kubadilishana na Wapalestina wanaoshikiliwa pamoja na wafungwa, ikiwa ni sehemu ya awamu ya kwanza ya mpango wa amani wa Donald Trump.

Makubaliano hayo yamepelekea usitishwaji wa mapigano kuanza kutekelezwa siku ya Ijumaa na kuongezeka kwa kiasi cha misaada kuingia Ukanda wa Gaza.

Mara tu awamu ya kwanza itakapokamilika, mazungumzo yanatarajiwa kuanza kwa awamu nyingine.

Pia unaweza kusoma

Mateka walioachiliwa

Makubaliano ya kusitisha mapigano yatafanya Hamas iwaachilie mateka wote 48 wa Israel na raia wa kigeni ambao walikuwa wanashikiliwa kwa miaka miwili ya vita, 20 tu kati yao ndio wamethibitishwa kuwa hai.

Wote isipokuwa mmoja walikuwa miongoni mwa watu 251 waliotekwa nyara wakati wa shambulio la kundi la Wapalestina kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo takriban watu wengine 1,200 waliuawa.

Israel ilijibu kwa kuanzisha mashambulizi huko Gaza, ambapo zaidi ya watu 67,000 wameuawa, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.

Siku ya Jumatatu asubuhi, Hamas iliwaachia mateka 20 katika makundi mawili na kuwakabidhi kwa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC).

Serikali ya Israel ilisema kundi la kwanza lilikuwa ni: Eitan Mor, Gali Berman, Ziv Berman, Omri Miran, Alon Ohel, Guy Gilboa-Dalal na Matan Angrest.

Kundi la pili: Bar Kupershtein, Evyatar David, Yosef-Chaim Ohana, Segev Kalfon, Avinatan Or, Elkana Bohbot, Maxim Herkin, Nimrod Cohen, Matan Zangauker, David Cunio, Eitan Horn, Rom Braslabski na Ariel Cunio.

Lakini si maiti zote ambazo zimeachiliwa.

Kulingana na nakala ya makubaliano ya kusitisha mapigano, maiti wote yanapaswa kukabidhiwa siku ya Jumatatu.

Lakini Hamas imethibitisha kwamba ni miili minne tu ndio imerejeshwa Israel siku ya Jumatatu – Guy Illouz, Yossi Sharabi, Bipin Joshi na Daniel Peretz.

“Tunaitaka Hamas kutekeleza makubaliano,” msemaji wa Israel alisema, akiongeza jeshi la Israel “halitapumzika hadi wote warudi kwa familia zao na kuzikwa nchini Israel.”

Haijabainika ikiwa mpango wa Trump ulibainisha kwamba Hamas na makundi mingine ya Palestina hayawezi kuipata miili yote katika muda uliowekwa.

Afisa wa Israel alisema hapo awali kwamba kikosi kazi cha kimataifa kitaanza kazi ya kutafuta mabaki ya mtu yeyote ambaye hajarejeshwa.

Wapalestina walioachiliwa

Kwa kubadilishana na mateka hao, Israel imekubali kuwaachilia wafungwa 250 wa Kipalestina wanaotumikia vifungo vya maisha katika jela za Israel na wanaoshikiliwa 1,718 kutoka Gaza, wakiwemo watoto 15.

Orodha ya majina ya Wapalestina ilichapishwa na Ofisi ya Habari ya Wafungwa inayoendeshwa na Hamas siku ya Jumatatu asubuhi.

Orodha ya wafungwa haijumuishi watu maarufu wanaotumikia vifungo vya maisha kwa mashambulizi mabaya dhidi ya Waisraeli – ikiwa ni pamoja na Marwan Barghouti na Ahmad Saadat – ambao Hamas ilitaka waachiliwe.

Vyombo vya habari vya Israel viliripoti wiki iliyopita kwamba karibu 100 kati ya 250 wataachiliwa katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel, 15 Jerusalem Mashariki inayokaliwa kwa mabavu, na 135 watapelekwa Ukanda wa Gaza au kwingineko.

Haijabainika iwapo kucheleweshwa kuachiliwa kwa mateka wote waliofariki kunaweza pia kuchelewesha kuachiliwa kwa wafungwa hao wa Kipalestina.

Nini kitatokea baadaye?

Kabla ya kuachiliwa kwa mateka hao, wanajeshi wa Israel walijiondoa Gaza na kukaa katika eneo linalowapa udhibiti wa asilimia 53 ya Gaza – hatua ya kwanza kati ya tatu za Israel kujiondoa, kulingana na mpango wa Trump.

Kikosi cha kimataifa cha takriban wanajeshi 200 wanaosimamiwa na jeshi la Marekani watafuatilia usitishaji huo wa mapigano, kulingana na afisa mkuu wa Marekani. Inaaminika kuwa kikosi hicho kinajumuisha wanajeshi kutoka Misri, Qatar, Uturuki na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Maafisa wa Marekani wamesema hakuna jeshi la Marekani litakaloinga Gaza.

Mpango wa Trump unasema Gaza itakongolewa kijeshi na “miundombinu yote ya kijeshi, ugaidi na mashambulizi” itaharibiwa.

Pia Gaza itasimamiwa na kamati ya muda ya mpito – inayosimamiwa na “Bodi ya Amani” inayoongozwa na Trump na kumshirikisha Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair.

Utawala wa Ukanda huo hatimaye utakabidhiwa kwa Mamlaka ya Palestina – ambayo inasimamia Ukingo wa Magharibi – mara tu itakapofanyiwa mageuzi.

Hamas – ambayo imetawala eneo hilo tangu 2007 – haitakuwa na jukumu lolote la moja kwa moja au lisilo la moja kwa moja katika kuitawala Gaza, kulingana na mpango huo.

Wapiganaji wa Hamas watapewa msamaha ikiwa watakubali kuishi pamoja kwa amani, au wataruhusiwa kwenda nchi nyingine.

Hakuna Mpalestina ambaye atalazimishwa kuondoka Gaza na wale wanaotaka kuondoka watakuwa huru kurudi tena.

Mpango wa maendeleo wa kuijenga upya Gaza utaundwa na jopo la wataalamu.

Maswali yasiyo na jawabu

Kuna uwezekano kuwa kuna mambo yataleta mvutano wakati wa mazungumzo juu ya awamu inayofuata ya mpango huo.

Hamas imekataa kuweka chini silaha zake, ikisema itafanya hivyo mara tu taifa la Palestina litakapoanzishwa.

Kundi hilo pia halikutaja mpango wa kuweka silaha chini katika majibu yake ya awali kwa mpango huo wikendi iliyopita, na hivyo kuchochea uvumi kwamba msimamo wake haujabadilika.

Ingawa Israel imekubali mpango wa Trump kwa awamu ya kwanza, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alionekana kukataa Mamlaka ya Palestina kuhusika katika Gaza baada ya vita.

Hamas pia imesema inatarajia kuhusika katika siku zijazo huko Gaza kama sehemu ya “vuguvugu la umoja la Wapalestina.”

Jambo jingine linaloweza kuleta mvutano ni uondokaji wa wanajeshi wa Israel. Israel inasema kujiondoa kwake kwa mara ya kwanza kutapelekea kubaki na udhibiti wa karibu 53% ya Gaza.

Lakini mpango wa White House unaonyesha uondokaji wa jeshi utafanya kuidhibiti Gaza kwa 40% na kisha 15%.

Maneno kuhusu kuondoka Jeshi la Israel hayaeleweki na hayatoi ratiba ya wazi ya kujiondoa kikamilifu kwa Israel – jambo ambalo Hamas wanaweza kutaka liwekwe wazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *