Dar es Salaam. Uamuzi wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria, Ezekiah Wenje, kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM), umeibua mitazamo miwili kinzani. Wapo wanaosema chama hicho cha upinzani kimepoteza, huku wengine wakiona ni mwendelezo wa kujisafisha.

Hoja ya wanaosema chama kimepoteza inajengwa katika msingi kwamba bado kunaonekana ndani ya chama hicho majeraha ya uchaguzi wa ndani uliofanyika Januari mwaka huu, hivyo baadhi ya wanachama hawana raha na chama chao.

Wanaiambatanisha hoja hiyo na kile ambacho wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema, ingawa kulionekana dalili za Wenje kuondoka, bado itabaki kuwa pigo kwa chama hicho, kwa kuwa alikuwa na wafuasi wengi hasa kutoka kanda yake.

Kwa upande wa wanaosema ni mwendelezo wa chama hicho kujisafisha, wanajenga hoja kwamba Wenje na wanachama wengine walioondoka walishaonekana dhamira yao, hivyo kuondoka kwake kunaacha pumzi safi.

Wamekwenda mbali zaidi kwa kueleza kwamba kuondoka kwa Wenje si pigo kama inavyodhaniwa, kwa kuwa wapo wengi wakubwa waliowahi kuondoka wakiwemo Zitto Kabwe na Willibrod Slaa, lakini chama hicho kikaendela kubaki imara.

Mitazamo hiyo kinzani inakuja siku moja tu baada ya Wenje kutangaza kuihama Chadema alikokuwepo kwa zaidi ya miaka 15 na kuhamia katika chama tawala.

Katika ufafanuzi wake, Wenje amesema amejiunga na CCM ili kuhakikisha anatumia uwezo na akili yake angali hai, kushauri masuala yatakayoijenga nchi, kwa kuwa chama hicho tawala ni jukwaa sahihi la kufanya hivyo.

 Ameambatanisha kauli yake hiyo na dongo alilolipiga kwa Chadema, akisema si kwamba kilizuiwa na Serikali kushiriki uchaguzi mkuu kama kinavyodai, bali kilikaa katika vikao vyake na kuamua kutoshiriki.

Anachokisema Wenje kinaakisi methali ya ‘maneno ya mkosaji’ au ndiyo uhalisia uliopo ndani ya chama hicho, wachambuzi wa masuala ya siasa wanafafanua kwa kina.

Imepoteza?

Kuondoka kwa Wenje ndani ya Chadema, kwa mujibu wa mchambuzi wa siasa, Said Majjid, ni maumivu kwa chama hicho, kwa kuwa mwanachama huyo alikuwa kiongozi wa kanda yenye watu wengi na hivyo aliungwa mkono nao.

Kwa kuwa walimuunga mkono kiasi cha kumchagua kuwa mwenyekiti wa kanda kwa zaidi ya mara moja, amesema kuna dalili ya kuwepo watakaomfuata kwa kile alichokiamua, hivyo watu wasishangae kusikia kundi la wanaomuunga mkono Wenje wamejiunga na CCM.

“Ni jambo la kawaida kwa sababu walishaondoka wanachama wengi wenye nguvu, lakini kupoteza kupo palepale. Kila mwenye nguvu anayeondoka, anapoteza kitu ndani ya chama husika,” amesema Majjid.

Ingawa kuna maneno mengi dhidi ya Wenje, amesema kuna umuhimu alikuwa nao ndani ya chama hicho. Kuthibitisha hilo, amechaguliwa mara kadhaa kuwa kiongozi tena kwa nafasi za juu.

“Kumbuka Wenje alikuwa mbunge mwaka fulani kupitia Chadema. Ukisema hana lolote unakosea. Alikuwa mbunge kwa sababu alipigiwa kura, watu humpigia mtu kura, sio chama. Kwa hivyo kuondoka kwake, maana yake kaondoka na sehemu ya watu wake,” amesema Majjid.

Majjid amesema anachokubaliana na wengi ni kwamba kuondoka kwa Wenje hakutasababisha kifo cha Chadema, kwa sababu mtu mmoja hatoshi kuangusha taasisi.

Hoja ya Chadema kupoteza inaungwa mkono na mchambuzi mwingine wa siasa, Dk Paul Loisulie, anayesema kuondoka kwa Wenje wakati huu inaendelea kuonesha picha jinsi uchaguzi uliofanyika ndani ya chama ulivyoacha vidonda.

Amesema kwa kuwa uchaguzi ulihusisha pande mbili, upande mmoja haukuridhika na matokeo hadi sasa kwa kuwa hawakuamini kama uchaguzi usingekuwa upande wao.

Kwa upande mwingine, amesema CCM itamtumia kada huyo wa zamani wa Chadema kwa faida, hasa kujibu mashambulizi ambayo chama hicho tawala kimekuwa kikielekezewa. Amesema CCM itamtumia Wenje kama silaha yake kujibu mambo yote ambayo chama hicho kinatuhumiwa nacho.

Ni kujisafisha?

Kwa upande mwingine, Dk Loisulie amesema kuhama kwa Wenje si jambo jipya kwani wapo viongozi walioondoka ndani ya chama hicho.

“Dk Wilbroad Slaa aliondoka Chadema, Zitto Kabwe aliondoka, kwa sasa hakuna jambo jipya watu wanaondoka na chama kinaendelea kubaki,” amesema.

Amesema kwa kuwa tayari kulishakuwa na tuhuma dhidi ya Wenje ndani ya chama hicho, kuondoka kwake kunazidi kukisafisha chama hicho cha upinzani. Zipo hasira za ndani, lakini kuondoka kwa Wenje ilikuwa ni suala la muda tu, kwa sababu tayari mwenyekiti Tundu Lissu alishamtaja kwa tuhuma mbalimbali.

Hoja hiyo haina tofauti na alichokisema mchambuzi wa siasa, Tumaini Mnale, aliyesema kilichofanywa na Wenje ni kudhihirisha kuwa yupo kwa maslahi zaidi na sio kile anachokiamini.

Amesema kuhama kwa viongozi ndani ya chama hakuna athari kubwa zaidi ya kuleta mshtuko, lakini wanachama wanapobaini rangi ya aliyekuwa kiongozi wao huwaamini wale wanaopigania maslahi ya wananchi na sio wale wanaopigania maslahi yao.

Amedokeza kuwa chama cha siasa kupoteza viongozi wake kwenda vyama vingine ni jambo la kawaida na chama huendelea kujijenga kwa kuwa mtaji wa chama ni wanachama. Amesisitiza kuhama chama ni uamuzi na hakuna uvunjwaji wa sheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *