Mwanasheria mkuu wa jimbo la New York, Letitia James, ambaye amefunguliwa mashtaka na wizara ya sheria ya Rais Donald Trump, ameibuka hadharani kwa msimamo thabiti na kumuunga mkono Zohran Mamdani, mgombea anayeongoza katika kinyang’anyiro cha umeya wa New York na mkosoaji mwingine mkali wa rais huyo wa Marekani. Akihutubia mkutano wa hadhara katika eneo la Washington Heights, Manhattan, James alisema hatamwogopa mtu yeyote, akionekana kumrejelea Trump kwa kauli yake: “I fear no man.”

James, mwenye umri wa miaka 66, anatuhumiwa kwa makosa ya udanganyifu wa benki na kutoa taarifa za uongo kwa taasisi ya kifedha, mashtaka yaliyowasilishwa na jopo la mahakama huko Alexandria, Virginia. Hapo awali, alikuwa ameongoza kesi iliyopelekea Trump kutozwa faini ya dola milioni 454 kwa kudanganya kuhusu thamani ya mali zake, ingawa faini hiyo ilifutwa baada ya rufaa huku hukumu ya awali dhidi ya rais huyo ikibaki.

USA New York mgombea umeya Zohran Mamdani
Mgombea umeya wa jiji la New York Zohran Mamdani amemsifu Letitia James kwa kusimama kidete dhidi ya Trump.Picha: Michael M. Santiago/Getty Images

Mamdani: Huu ndiyo wakati wetu wa kupigania haki

Katika mkutano huo, Mamdani, kijana mwenye umri wa miaka 33 na mwanasiasa wa mrengo wa kisoshalisti, alimpongeza James kwa “uamuzi wa kusimama kidete” akisema, “Huu ndiyo wakati wetu wa kupigania haki, kwani utawala wa kiimla wa sasa unalipiza kisasi dhidi ya wote waliothubutu kumpinga.” Kura za maoni za hivi karibuni kutoka Chuo Kikuu cha Quinnipiac zinaonyesha Mamdani anaongoza kwa tofauti ya pointi 13 dhidi ya mpinzani wake wa karibu, aliyewahi kuwa gavana, Andrew Cuomo.

Mashtaka dhidi ya James yameibuka siku moja tu baada ya James Comey, aliyewahi kuwa mkurugenzi wa FBI na mkosoaji mwingine wa Trump, kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kwa Bunge la Marekani. Wanasheria wakuu 22 kutoka majimbo kadhaa ikiwemo California, Illinois na Washington wamelaani mashtaka hayo wakisema ni “mfano wa matumizi mabaya ya mamlaka ya kisheria” na kwamba vitendo hivyo “ni alama za tawala za kiimla, si demokrasia ya Marekani.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *