
Mfalme Abdullah II wa Jordan ameonya kuwa Mashariki ya Kati itaangamia iwapo hakutakuwa na mchakato wa amani utakaopelekea taifa la Palestina.
Mfalme huyo alikuwa akizungumza katika mahojiano maalum na Panorama ya BBC, alipokuwa akijiandaa kuhudhuria mkutano wa kilele katika Sharm el-Sheikh nchini Misri kuhusu mpango wa amani wa Rais Donald Trump wenye pointi 20 katika eneo hilo.
Mkutano huo unafanyika siku ambayo Hamas iliwaachilia huru mateka wa mwisho wa Israel waliokuwa wanashikiliwa huko Gaza kwa kubadilishana na wafungwa wa Kipalestina na wafungwa wanaoshikiliwa na Israel.
“Ikiwa hatutatatua tatizo hili,” Mfalme Abdullah alisema, “kama hatutapata mustakabali wa Waisraeli na Wapalestina na uhusiano kati ya ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu na Israeli, tutaangamia.”
Mfalme Abdullah amesema eneo hilo limeshuhudia majaribio mengi ya kutafuta amani yaliyofeli na kwamba utekelezaji wa suluhisho la mataifa mawili – kuundwa kwa taifa huru la Palestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Gaza, pamoja na Israel – ndilo jibu pekee.
“Natumai tunaweza kurudisha mambo nyuma, lakini kwa mtazamo wa kisiasa, kwa sababu tusipotatua shida hii, litajirudia tena,” mfalme alisema.
Serikali ya sasa ya Israel imekataa mara kadhaa suluhisho la serikali mbili. Katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwezi uliopita, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisisitiza upinzani wake.
“Kwa hakika, walikuwa na taifa la Palestina – huko Gaza. Walifanya nini na jimbo hilo? Amani? Kuishi pamoja?”
“Hapana, walitushambulia mara kwa mara, bila kuchokozwa, walirusha maroketi katika miji yetu, waliua watoto wetu, waligeuza Gaza kuwa kituo cha ugaidi ambako walifanya mauaji ya Oktoba 7,” aliongeza, akimaanisha mashambulizi yaliyoongozwa na Hamas miaka miwili iliyopita ambayo yalianzisha mzozo huu wa Gaza.
Hata hivyo, ni katika mkutano huo huo wa Umoja wa Mataifa ambapo Rais Trump alimwita Mfalme Abdullah na viongozi wengine wa eneo hilo kwenye mkutano ili kuelezea mpango wake wa amani.
“Ujumbe alioutoa kwetu sisi sote ulikuwa kwamba, ‘Hii lazima ikome. Inabidi ikome sasa.’ Na tukasema, ‘Unajua, Bw Rais, kama kuna mtu yeyote anaweza kufanya hivyo, ni wewe,'” Mfalme Abdullah alisema.
Akirejelea ghasia za miaka miwili iliyopita, ikiwa ni pamoja na vita vya Israel na Iran na shambulio la Israel dhidi ya viongozi wa Hamas nchini Qatar mwezi uliopita, Mfalme Abdullah aliuliza: “Je, tumekaribia kwa kiasi gani katika eneo, ikiwa si mzozo wa pande za kusini na kaskazini ambao ungezunguka dunia nzima?”

Akimzungumzia Netanyahu, kiongozi huyo wa Jordan alisema “haamini kitu anachosema”. Lakini aliamini kuna Waisraeli ambao viongozi wa Kiarabu wangeweza kufanya nao kazi kujenga amani.
Kuhusu Hamas na kukubali kwake kukabidhi utawala wa Gaza kwa chombo huru cha Palestina chini ya masharti ya makubaliano ya kusitisha mapigano, mfalme alisema amehakikishiwa na wale “wanaofanya kazi karibu nao, Qatar na Misri, [ambao] wanahisi matumaini makubwa sana kwamba watatii hilo.”
Lakini mfalme alionya kwamba “shetani alikuwa katika undani” wa makubaliano ya upatanishi ya Trump, na kwamba mara tu usitishaji wa mapigano utakapopatikana huko Gaza ni muhimu kwamba rais wa Marekani aendelee kujishughulisha na mchakato huo.
“Katika mazungumzo yetu na Rais Trump, anajua kwamba sio Gaza pekee, sio tu upeo fulani wa kisiasa. Ninamaanisha kuwa anaangalia kuleta amani katika eneo zima. Hilo halitafanyika isipokuwa iwapo Wapalestina watakuwa na mustakabali.”

Jordan imekuwa na mkataba wa amani na Israel tangu mwaka 1994, licha ya upinzani kutoka kwa watu wengi nchini humo. Zaidi ya asilimia 50 ya wakazi wa nchi hiyo wana asili ya Kipalestina. Nchi hizo mbili zinashirikiana katika baadhi ya masuala ya usalama.
Amani hiyo ilikubaliwa na marehemu babake mfalme wa sasa, Mfalme Hussein, na waziri mkuu wa Israel marehemu Yitzhak Rabin. Rabin aliuawa na Myahudi mwenye msimamo mkali mwaka uliofuata. Nilimuuliza Mfalme Abdullah ikiwa anaamini ataona makubaliano ya mwisho ya amani ikiwa ni pamoja na nchi ya Palestina ndani ya maisha yake mwenyewe?
“Lazima ifanyike , kwa sababu njia mbadala ingemaanisha kuangamia kwa eneo hili. Baba yangu, nakumbuka kuelekea mwisho wa maisha yake, alikuwa akisema, ‘Nataka amani kwa watoto wangu na watoto wao.’ Nina wajukuu wawili;
“Na nadhani hilo ndilo linalonitia moyo mimi na wengi wetu katika eneo hili, kwamba amani ndiyo chaguo pekee. Kwa sababu ikiwa haitatokea, mara ngapi Magharibi na Marekani zinaburutwa katika hili? Imekuwa miaka 80. Na nadhani ni wakati wa sisi sote kusema inatosha.”
Zaidi ya watu 67,000 wameuawa na jeshi la Israel huko Gaza tangu tarehe 7 Oktoba 2023, kulingana na maafisa wa wizara ya afya katika eneo linaloongozwa na Hamas.
Historia haitoi sababu nyingi za matumaini, lakini Mfalme Abdullah anaamini huu ni wakati wa uwezekano wa kweli.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla