Rais wa zamani wa Russia, Dmitry Medvedev, amesisitizia haja ya kuundwa taifa huru la Palestina na kutambuliwa uwepo wa nchi huru ya Palestina duniani akisema kuwa, vita haviwezi kumalizika ila kwa kuundwa nchi huru ya Palestina.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars; rais huyo wa zamani wa Russia ambaye hivi sasa ni Naibu wa Mkuu wa Baraza la Usalama la Russia, alisema hayo jana wakati akizungumzia suala la mabadilishano ya mateka kati ya Palestina na utawala wa Kizayuni na kuongeza kuwa, hatua hii ya kubadilishana mateka haitatatua chochote kwani utatuzi wa kadhia ya Palestina ni kuundwa nchi huru ya Palestina na kutambuliwa rasmi duniani.

Amesema hayo kwenye ujumbe wake katika mtandao wa kijamii wa X na kuandika: “Kuachiliwa huru mateka wa Israel na Palestina, bila ya shaka, ni jambo zuri, lakini halitotatua chochote.”

Rais huyo wa zamani wa Russia vilevile amesema: “Maadamu nchi huru na kamili ya Palestina haijaundwa kama yanavyosema maazimio yanayotambuliwa na Umoja wa Mataifa, basi hakuna kitakachobadilika. Vita vitaendelea. Kila mtu anaelewa hili.”

Nchi nyingi duniani zimesisitizia haja ya kuanzishwa nchi huru ya Palestina. Hivi karibuni nchi za Ulaya nazo zimelitambua suala hilo, lakini Marekani na utawala wa Kizayuni zinaendelea kukwepa kukubali suala hilo na kulitekeleza kivitendo.

Kwa upande mwingine, viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wanaendelea kung’ang’ania mara kwa mara kwamba watafanya kila wawezako kuzuia kuundwa nchi huru ya Palestina.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *