
Chanzo cha picha, Getty Images
Katika hatua iliyozua mjadala ndani na nje ya Misri, Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri amemtunuku Rais wa Marekani, Donald Trump, Nishani ya Nile (Order of the Nile), ambayo ni heshima ya juu kabisa ya kiraia nchini humo, kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Ikulu ya Rais.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa tuzo hiyo imetolewa kwa Trump kwa “kutambua mchango wake wa kipekee katika juhudi za kuleta amani na kutatua migogoro, hasa nafasi yake muhimu katika kusitisha vita vya Gaza.”
Uamuzi huo uliambatana na mkutano wa kilele ulioandaliwa na marais hao wawili huko Sharm el-Sheikh, ambapo zaidi ya viongozi ishirini walishiriki kujadili amani ya Mashariki ya Kati.
Lakini, mkufu wa Nile ni nini hasa? Na ni vigezo gani vinazingatiwa ili kutunukiwa tuzo hiyo?
Mkufu wa Nile: Historia na umuhimu wa kiheshima
Mkufu wa Nile ni tuzo ya juu kabisa ya kiraia inayotolewa na Jamhuri ya Misri.
Ilianzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1915, wakati wa utawala wa Sultani Hussein Kamel, kwa ajili ya kuwatuza watu waliotoa huduma za kipekee kwa Misri au kwa ubinadamu kwa ujumla.
Baada ya Mapinduzi ya Julai 1952 na kutangazwa kwa mfumo wa jamhuri, mfumo mzima wa tuzo ukafanyiwa mabadiliko makubwa.
Mkufu wa Nile ukapewa hadhi ya kuwa tuzo ya juu zaidi nchini, inayotolewa moja kwa moja kwa maamuzi ya Rais wa Jamhuri kwa wakuu wa nchi au watu mashuhuri waliotoa mchango mkubwa wa kibinadamu, kitamaduni au kijamii.
Kwa mujibu wa Sheria ya Misri Na. 12 ya mwaka 1972, tuzo hiyo hutolewa kwa wale wanaotoa huduma za kipekee kwa taifa au kwa ubinadamu.
Walengwa huwa ni wakuu wa nchi au watu mashuhuri wa kimataifa katika nyanja za sayansi, fikra, au diplomasia.
Tuzo hiyo huambatana na cheti rasmi kilichosainiwa na Rais wa Jamhuri na kuandikishwa katika kumbukumbu rasmi za taifa.
Kwa miongo mingi, Mkufu wa Nile umebeba taswira ya shukrani na heshima ya juu kutoka kwa taifa la Misri kwa watu waliosaidia maendeleo yake au kulisaidia kuimarika kimataifa.
Kwa namna hiyo, tuzo hii imepewa maana pana ya kiishara.

Chanzo cha picha, Photoshot
Muundo na maana ya mkufu wa Nile
Mkufu huu hutengenezwa kwa dhahabu safi au fedha iliyopakwa dhahabu.
Muundo wake unaakisi urithi tajiri wa ustaarabu wa kale wa Wamisri.
Mkufu huundwa kwa vipande vya mraba vilivyopambwa kwa enameli yenye rangi na alama za kifarao.
Vipande hivi vinaunganishwa na minyororo miwili ya sambamba, iliyopambwa na maua ya yungiyungi ya Misri – ishara ya usafi na umilele katika tamaduni ya Misri ya kale.
Katikati ya shanga hiyo, kunaning’inia medali kubwa ya mviringo inayoashiria mto Nile- chanzo cha uhai na ustaarabu wa Misri.
Tuzo hiyo hutolewa katika hafla rasmi ndani ya ikulu, ambapo Rais mwenyewe humkabidhi mhusika.
Na iwapo mhusika atafariki dunia, hufanyiwa hafla ya kitaifa kwa mujibu wa itifaki ya kijeshi.
Waliowahi kutunukiwa Shanga ya Nile
Katika historia yake, mkufu wa Nile umetolewa kwa viongozi na watu mashuhuri wa kimataifa waliotoa mchango mkubwa katika kuimarisha amani, ushirikiano au maendeleo ya ubinadamu.
Mwaka 1979, Rais Anwar Sadat alimtunuku Rais Jimmy Carter wa Marekani tuzo hiyo kwa mchango wake mkubwa katika kufanikisha makubaliano ya amani kati ya Misri na Israel.
Kiongozi wa zamani wa Yugoslavia, Josip Broz Tito, alikuwa mmoja wa viongozi wa kwanza wa kigeni kupokea tuzo hiyo mwaka 1955 chini ya Rais Gamal Abdel Nasser, kwa mchango wake katika kuasisi Harakati ya Kutokupendelea Upande Wowote.
Mwaka 1975, Malkia Elizabeth II alipokea tuzo hiyo wakati wa ziara yake rasmi nchini Misri.
Mwaka uliofuata, Rais Sadat alimtunuku Sultan Qaboos bin Said wa Oman kwa mchango wa nchi yake wakati wa vita vya Oktoba 1973.
Nelson Mandela alitunukiwa Shanga ya Nile mwaka 1990 kwa kupambana na ubaguzi wa rangi Afrika Kusini.
Katika mwaka huo huo, Rais Hosni Mubarak alimkabidhi Mfalme Akihito wa Japan tuzo hiyo kama ishara ya urafiki kati ya Misri na Japan.
Katika miaka ya hivi karibuni, waliopokea tuzo hii ni pamoja na Mfalme Salman bin Abdulaziz wa Saudi Arabia, Mfalme Hamad bin Isa Al Khalifa wa Bahrain, na Rais Mohamed Ould Abdel Aziz wa Mauritania – wakionyesha uhusiano wa karibu wa kihistoria kati ya nchi hizo na Misri.
Kwanini Trump ametunukiwa Tuzo hii sasa?
Uamuzi wa kumtunuku Rais Donald Trump mkufu wa Nile umetokana na muktadha wa kisiasa na kidiplomasia wa sasa.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Ikulu ya Rais, tuzo hiyo imetolewa kwa kutambua “mchango wake katika kuendeleza juhudi za amani na kupunguza migogoro, hasa nafasi yake muhimu katika kusitisha vita ya Gaza.”
Trump alisimamia mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Israel na Hamas yaliyofanikisha makubaliano ya kusitisha vita, ambayo yaliratibiwa kwa ushirikiano na Misri, Marekani na Qatar.
Mafanikio haya yaliipa Misri nafasi ya kuimarisha nafasi yake kama mpatanishi mkuu katika mzozo wa Palestina.
Tukio la kutunuku tuzo hii limeambatana na mkutano wa kimataifa wa amani unaofanyika Sharm el-Sheikh, ulioandaliwa kwa pamoja na Rais Sisi na Trump, na ambao umewahusisha zaidi ya viongozi ishirini kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Sifa, mabishano na ukosoaji
Uamuzi huo haukupita kimya kimya.
Wakati baadhi waliuona kama ishara ya kutambua juhudi za amani, wengine walikosoa uamuzi huo, wakidai kuwa unaipunguzia tuzo hiyo heshima yake ya kihistoria kwa kuingizwa katika muktadha wa kisiasa wa muda mfupi.
Katika mitandao ya kijamii, mjadala mkali uliibuka.
Baadhi waliona uamuzi huo kama ishara ya uhuru wa maamuzi wa Misri na uwezo wake wa kuwatuza wanaochangia uthabiti wa kikanda.
Wengine waliona kama ishara ya kujipendekeza kwa Marekani, hali inayodhoofisha maana ya kitaifa ya tuzo hiyo.
Hatimaye, Mkufu wa Nile – uliyokuwa na uzito wa heshima ya dhahabu – uligeuka kuwa mada ya utani na kejeli miongoni mwa wananchi, huku baadhi wakisema kuwa “utukufu uliobebwa na majina kama Nelson Mandela na Jimmy Carter” unafifia inapopewa kiongozi mwenye utata kama Donald Trump.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid