Mkutano wa Tatu na G20 wa mwisho wa Kikosi Kazi cha Mazingira na Ulinzi Endelevu wa Hali ya Hewa (ECSWG) ulifunguliwa rasmi jana Jumatatu mjini Cape Town, Afrika Kusini.

Akifungua mkutano wa huo ECSWG, Waziri wa Misitu, Uvuvi na Mazingira wa Afrika Kusini, Dion George alisema kuwa, mambo yatakayojadiliwa kwenye kikao hicho wiki hii itaweka msingi wa kupitishwa tamko la mawaziri la ECSWG ambalo pia litajulikana kama Azimio la Cape Town.

Kwa mujibu wa waziri huyo, tamko hilo litatilia mkazo ahadi tatu: kuharakisha utekelezaji wa mikataba iliyopo ya kimataifa; kuimarisha ushirikiano kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea kupitia fedha, teknolojia na usaidizi wa uwezo na kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika maeneo yote ya hatua za mazingira.

Katika kipindi cha wiki nzima, wajumbe watajadili maeneo sita muhimu zaidi ambayo ni: bioanuwai na uhifadhi; uharibifu wa ardhi, hali ya jangwa, ukame na uendelezaji wa vyanzo vya maji; kemikali na usimamiaji wa takataka; mabadiliko ya hali ya hewa; ubora wa hewa na masuala yanayohusiana na bahari na fukwe.

Matokeo ya Mkutano wa G20 unaoendelea hadi Jumatano, yatatangaza maamuzi katika Mkutano wa Mawaziri wa G20 kuanzia Alkhamisi hadi Ijumaa na kuingia kwenye Mkutano wa Viongozi wa G20 mwishoni mwa mwezi ujao.

Hata hivyo, umoja wa dhamira katika mkutano wa Cape Town umekumbwa na changamoto kufuatia matamshi ya Usha-Maria Turner, mkuu wa ujumbe wa Marekani ambaye amesema nchi yake haiungi mkono rasimu ya tamko la Ajenda ya Umoja wa Mataifa ya 2030 ya Maendeleo Endelevu au Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *