Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi, amepokewa na tatizo la fidia kwa wananchi wa Jimbo la Dimani, akiahidi kuunda tume ya kuhakiki upya maeneo yote yaliyopitiwa na miradi jimboni humo ili kupata uhalisia na kuhakikisha kila mmoja anapata stahiki zake.

Amesema iwapo mwananchi atadhulumiwa, dhima hiyo anaibeba yeye na hayupo tayari kuona jambo hilo likitokea licha ya umuhimu wa kuwa na miradi ya maendeleo.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni na makundi mbalimbali jimboni Dimani leo Oktoba 14, 2025, kwenye Uwanja wa Mpira wa Dimani, Mkoa wa Mjini Magharibi, Dk Mwinyi amesema maendeleo yanakwenda sambamba na changamoto, lakini ni lazima watu wapate haki zao.

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk Hussein Mwinyi akizungumza na makundi mbalimbali Jimbo la Dimani katika uwanja wa mpira Dimani ukiwa ni mwendelezo wa Kampeni zake

“Nawapa ahadi ya kuunda tume ya kuja kuhakiki fidia ambazo zimetayarishwa. Kilio kikubwa hapa ni fidia, kwa hiyo tutakuja kuhakiki watu walilipwa nini na wanastahili kulipwa nini ili tuliweke sawasawa,” amesema.

Hata hivyo, amesema wapo watu wanaposikia kuna miradi inajengwa, wanakwenda haraka kujenga nyumba na kuweka vipando ili walipwe fidia kubwa.

“Kwa hiyo ndugu zangu, tusaidiane. Hili suala la watu kujenga foundation (misingi) usiku tuache,” amesema na kueleza kuwa kuna wakati fidia inakuwa kubwa kuzidi thamani ya miradi inayojengwa.

“Lakini ninachoweza kusema, mtu yeyote kudhulumiwa nitabeba mimi dhima. Nitahakikisha mtu hadhulumiwi. Kwa hiyo, tusaidiane kuwatambua hata wale wajanja wajanja wanaposikia miradi inakuja wanajileta kuendeleza maeneo yao,” amesema.

Dk Mwinyi amesema lengo la Serikali ni kumwondolea umaskini mwananchi na si kumwongezea.

“Tunachotaka sisi ni mtu tumtoe sehemu, aende sehemu nyingine afaidike, lakini siyo kumtia umaskini ili kesho na keshokutwa aishukuru Serikali na si kulalamikia Serikali,” amesema.

Wananchi wa Jimbo la Dimani wakiwa katika mkutano wa Kampeni na mgonbea urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk Hussein Mwinyi katika uwanja wa mpira Dimani Mkoa wa Mjini Magharibi

Amesema si haki kwa Serikali kutengeneza miji yake halafu watu wasipate fidia inayokwenda na hali halisi.

Amewataka viongozi wote kuanzia ngazi ya shehia hadi mkoa, wanaotaka kufanya miradi, waende kuzungumza na wananchi na kuchukua picha ili iwe rahisi kutambua wenye stahiki zao.

Mkazi wa Fumba, Abdallah Majura, amesema wanapaswa kutoa elimu kuhusu uwekezaji unaofanywa kwani kumekuwapo utaratibu wa kuibuka kwa miradi bila taarifa.

“Wananchi wa Fumba hatupingi maendeleo wala uwekezaji, lakini unapoamka asubuhi unakutana na alama bila kuelezwa kuna kitu gani,” amesema.

Amesema kuna watu nyumba zao zimewekwa alama lakini haijulikani kitu gani kinaendelea, hivyo ameomba ifanyike tathmini upya ili watu wapate wanachostahili.

Akizungumza kwa niaba ya wanaodai fidia wa Bweleo, Ali Mwinjuma Kilobo, amesema kuna haja ya watendaji kuwa karibu na wananchi wanapotekeleza miradi.

“Hili ni tatizo linalohitaji kutupiwa ufumbuzi, kinachofanyika ni kumtia mtu umaskini, ujinga na maradhi, ilhali wakati yanafanyika Mapinduzi na kuleta uhuru, viongozi wetu walitaka kuondoa vitu hivyo,” amesema.

Mkazi wa Bweleo, Mahmoud Ali Hamad, amesema wameathiriwa na mradi wa Chuo cha Teknolojia cha India (IIT Madras) bila kulipwa fidia zao.

“Tumeharibiwa vipando vyetu, nyumba zetu bila taarifa. Tunaomba tulipwe fidia kwa kuzingatia ardhi na vipando vyetu maana tumepata hasara kubwa. Watendaji wako wanafanya mambo bila kuzingatia sheria,” amesema.

Kwa upande wake, Asha Haji amesema: “Tunaomba tuangaliwe kwa jicho la pili, tena kwa huruma, maana tumeathiriwa sana.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *