Makubaliano ya amani ya Trump, licha ya madai ya Netanyahu kuwa ni “ushindi,” yamewakasirisha Wazayuni wengi.
Baada ya miaka miwili ya jinai na mauaji ya kimbari huko Gaza, utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mara nyingine tena umelazimika kusimamisha mashambulizi yake. Trump pia amemkumbusha Netanyahu kwa mara ya kadhaa kwenye mtandao wake wa kijamii kwamba vita vimekwisha.
Kulingana na Pars Today, hata hivyo, sauti tofauti zinasikika kutoka ndani ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu (Israel). Wengi wamekerwa na usitishaji vita uliowekwa na wanaona kuwa ni ishara ya kushindwa. Wakati Netanyahu akizungumza katika hotuba yake ya “usiku wa kusisimua na furaha,” wengine wamepinga kusherehekewa kwa makubaliano hayo ya usitishaji vita.
Kejeli na kuzomewa Netanyahu na Wazayuni wakati wa hotuba ya Steve Witkoff, mjumbe maalumu wa Ikulu ya White House katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ni ishara nyingine ya mgawanyiko mkubwa baina ya Waisraeli kuhusiana na makubaliano yaliyopo na kuyapachika chapa ya “ushindi.”
Ukweli kwamba Israel ilitwishwa makubaliano haya na Marekani limekuwa jambo la kuchukiza kiasi kwamba, baadhi wamekataa kuhudhuria hotuba ya Trump katika Bunge la Israel Knesset. Tovuti ya Israel National News imeandika: Avi Maoz Mwenyekiti wa Chama cha Noam ametangaza kwamba hatahudhuria hotuba ya Rais wa Marekani katika Bunge la Israel Knesset. “Utalazimika kuwa kipofu kabisa ili kuamini kwamba kutapatikana kitu kizuri katika mpango wa Trump.

Gazeti la Times of Israel pia limeripoti kwamba, mmoja wa wanachama wa chama cha Netanyahu amesusia hotuba ya Trump katika Knesset, akisema kuwa mpango wake ulikuwa “ndoto za alinacha.” Amit Halevi alisema: “Hotuba ya Trump ni ndoto za ushindi na maonyesho ya uongo. Siwezi kuhudhuria mkutano wa bunge na Rais wa Marekani Donald Trump na timu yake. Mpango huu ni kinyume cha ushindi.
“Lazima tuwaambie wananchi ukweli na kuinamisha vichwa vyetu kwa maumivu na aibu mbele ya kushindwa huku kijeshi. Hatupaswi kufanya mkutano wa hadhara chini ya jina la ushindi, ambao umejaa udanganyifu na maonyesho ya uongo.”
Limor Son Har-Melech, naibu spika wa bunge la utawala wa kizayuni wa Israel, pia aliandika katika chapisho la X akisusia hotuba ya Trump: “Trump aliwasilisha makubaliano ya sasa kama makubaliano ya amani! Lakini haya si makubaliano ya amani, bali ni makubaliano ya fedheha. Kinachokosekana ndani yake zaidi ya yote ni amani na usalama. Usalama wa Israeli umepata pigo kubwa kwa kutiwa kwake saini, na tayari tunaweza kuona Hamas ikijipanga upya katika Ukanda wa Gaza.”
Wachambuzi wa Israel wanaamini kwamba, mwisho wa vita vya Gaza, ni kama vile mwisho wa vita vya Israel dhidi ya Iran, ambapo Tel Aviv ililazimishwa na Marekani, na kwamba Israeli hatimaye italazimika kulipa gharama kubwa ya mwisho huu.