Mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amesema anajivunia kutekeleza dhamira ya mtangulizi wake, John Pombe Magufuli ya kuleta mabadiliko ndani ya nchi.
Akizungumza Oktoba 13, 2025 wakati wa mkutano wake wa kampeni uliofanyika mkoani Geita, Samia amesema kuwa miradi mingi mikubwa ya maendeleo aliyoianzisha Magufuli ameikamilisha.
“Nyote mtakubaliana na mimi nimetekeleza dhamira yake na shauku yake ya kuleta mabadiliko ndani ya nchi yetu,” alisema Samia.
Kulingana na Samia, mtangulizi wake alimuachia ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme wa Maji la Julius Nyerere (JNHPP) ukiwa katika asilimia 37 na sasa amelikamilisha na kuzalisha umeme.