Mchakato usikilizwaji wa kesi ya madai inayolikabili Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), iliyofunguliwa na Kocha Liston Katabazi akihoji uhalali wa kanuni za maadili zilizotumika kumuadhibu kifungo cha  maisha kutojishughulisha na soka, sasa umeanza rasmi upya.

Tayari Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu, imetoa hati za wito kwa wadaiwa, wadhamini waliosajiliwa wa TFF na TFF yenyewe ikiwataka kufika mahakamani hapo kwa ajili ya kujitetea.

Kwa mujibu wa hati hizo za wito kwa wadaiwa zilizosainiwa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Hakimu Mkazi Mkuu  Franco Kiswaga, Oktoba 13, 2025, kesi hiyo imepangwa Oktoba 21, 2025, saa 3:00 asubuhi.

“Unatakiwa kufika katika mahakama hii bila kukosa na siku hiyo unatakiwa kutoa nyaraka zako zote unazokusudia kuzitimia katika kesi yako”, zinasomeka hayo hizo ambazo pia TFF ilizipokea jana hiyo.

Hatua hiyo ya Mahakama ya Kisutu kuanza upya mchakato wa usikilizwaji wa kesi hiyo ni utekelezaji wa maelekezo na amri ya Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam.

Mahakama Kuu iliiamuru mahakama hiyo kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo baada ya kukubali rufaa aliyoikata Katabazi kupinga uamuzi huo wa Kisutu ulioitupilia mbali kesi hiyo awali.

Katabazi anayejitambulisha kuwa ni mdau wa soka na kocha wa mchezo huo mwenye leseni ya daraja C iliyotolewa na TFF alifungiwa na TFF kujishughulisha na soka ndani na nje ya nchi maisha yake yote, mwaka 2021.

Alifungiwa baada ya kuliandikia BMT barua Juni 15, 2021 akiishtaki TFF kuwa imeshindwa kusimamia mchezo huo kulingana na sheria, kanuni na miongozo yake.

Alipoitwa katika Kamati ya Maadili hakuhudhuria akijibu kuwa yeye si mwanachama wa Chama cha Makocha Tanzania (Tafca) ambacho kiko chini ya usimamizi wa TFF, hivyo si mwanachama wa TFF.

Juni 24, 2021 TFF ilichapisha katika tovuti yake uamuzi wa kumfungia Katabazi maisha kujishughulisha na masuala ya soka ndani na nje ya nchi.

TF 01

Hata hivyo, mwaka 2024 Katabazi alifungua kesi katika Mahakama ya Kisutu dhidi ya TFF na wadhamini wake akipinga uamuzi na adhabu hiyo .

Katika kesi hiyo ya madai namba 14708/2024,  alidai kuwa Kamati ya Maadili ya TFF haikuwa na mamlaka ya kumpa adhabu hiyo kwani Kanuni za Maadili za TFF, Toleo la Mwaka 2021, zilizotumika kumfungia si halali.

Alidai kuwa kanuni hizo hazijasajiliwa na BMT kwa mujibu wa matakwa ya Sheria namba 12 ya mwaka 1967 na marekebisho yake, na hivyo kuzifanya kuwa batili kutumika kwa wanachama wake na mtu mwingine yeyote.

Pia alidai kuwa amri hiyo iliingilia haki yake ya kufanya kazi katika nyanja ya soka na hivyo kumkosesha fursa ya kupata mshahara na kipato kwa ajili ya kuendeleza maisha yake ya kila siku na familia yake, na kumsababishia maumivu ya kisaikolojia.

Hivyo aliiomba mahakama iiamuru TFF imlipe Sh600 milioni kama fidia ya madhara ya jumla aliyoyapata kutokana na uamuzi wa kumfungia maisha uliotolewa kwa makusudi, kimakosa na kwa nia ovu.

Pia aliomba alipwe Sh100 milioni kama fidia ya adhabu kwa kitendo cha wadaiwa kutoa uamuzi huo wakijua kuwa hawana mamlaka ya kisheria kumchukulia hatua hiyo, riba ya kiwango cha Mahakama kwa tuzo (fedha ambazo ingeamuriwa alipwe) na gharama za kesi.

Vilevile aliiomba mahakama itoe zuio la matumizi ya Katiba na Kanuni za Maadili za TFF, akidai kuwa si vyombo halali kwa kutokusajiliwa kwa utaratibu na unaofaa.

Mahakama ya Kisutu katika uamuzi wake uliotolewa na Hakimu Kiswaga, iliifuta kesi hiyo, kufuatia pingamizi la awali lililoibuliwa na TFF.

Miongoni mwa vielelezo alivyoviwasilisha  mahakamani Kocha Katabazi ni barua ya BMT ya Juni 13, 2022 iliyothibitisha kuwa yeye si mwanachama wa TFF.

Hata hivyo, Hakimu Kiswaga ameamua kuwa Katabazi ni mwanachama wa TFF na kuwa kwa Katiba ya TFF alipaswa kukata rufaa Kamati ya Rufaa ya Maadili, na asingeridhika anaweza kwenda Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).

Hivyo amesema kuwa, kwa kuwa Katabazi hakufuata utaratibu huo, mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Katabazi alikata rufaa Mahakama Kuu akiwakilishwa na wakili Peter Majanjara pamoja na sababu nyingine, akidai kuwa  pingamizi la wajibu rufani halikuwa na msingi wa kisheria kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa kwenye pingamizi hilo.

Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Butamo Jaji Phillip Septemba 26, 2025, ilikubaliana na rufaa hiyo, hivyo ikatengua uamuzi wa Kisutu, ikaiamuru jalada lirejeshwe Kisutu iendelee kusikiliza madai ya msingi.

Amesema kuwa Mahakama ya awali (Kisutu) ilijihusisha na kutafsiri masharti ya Katiba ya TFF na matumizi yake na hivyo  ikaamua kwamba mrufani ni mwanachama wa TFF, ilhali yeye alikana kuwa si mwanachama wa TFF, hivyo hakufungwa na kanuni zake.

Amesema kuwa kwa kuangalia hati ya madai, haikuwa sahihi kwa ya Kisutu kukubali pingamizi la awali la mamlaka ya mahakama lililowekwa na wajibu rufani, kwani baadhi ya hoja zilihitaji kuthibitishwa kwa ushahidi.

Amefafanua kuwa mahakama hiyo ilipaswa kuchambua nyaraka zilizoambatanishwa kwenye hati ya madai baada ya kupokewa kama vielelezo ili kubaini baadhi ya mambo muhimu kuhusiana na madai ya mrufani kama vile uanachama wake katika TFF ili kufanya uamuzi sahihi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *