
Rais wa Marekani Donald Trump ameongoza kusainiwa kwa tamko jipya la amani linalolenga kudumisha usalama na utulivu katika Ukanda wa Gaza, akilita “siku kubwa kwa dunia na Mashariki ya Kati.” Makubaliano hayo yalisainiwa mjini Sharm el-Sheikh, Misri, yakihusisha viongozi wa Misri, Qatar na Uturuki kama wadhamini wa mpango wa kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas. Hatua hiyo imekuja saa chache baada ya pande hizo mbili kubadilishana mateka na wafungwa, hatua iliyopokelewa kwa shangwe katika Tel Aviv, Ramallah na Gaza.
Trump alifanya ziara ya ghafla nchini Israel, ambapo alilihutubia bunge la nchi hiyo na kumpongeza Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kwa “uongozi wa ujasiri” kabla ya kuelekea Misri kwa mkutano wa kilele wa Gaza. Akizungumza mbele ya zaidi ya viongozi 20 wa dunia, Trump alisema, “Tumefanikisha kile ambacho kila mtu alisema hakiwezekani. Hatimaye, tunayo amani katika Mashariki ya Kati.”
Ahadi ya viongozi kwa Gaza
Kulingana na tamko lililotolewa na Ikulu ya White House, nchi washiriki zimeahidi “kuendeleza dira jumuishi ya amani, usalama na ustawi wa pamoja katika eneo la Mashariki ya Kati.” Hata hivyo, waraka huo haukuweka wazi mustakabali wa suluhisho la taifa moja au mawili, jambo lililozua maswali kuhusu mwelekeo wa kisiasa wa mpango huo. Trump aliwaambia waandishi wa habari, “Tunazungumza kuhusu kujenga upya Gaza — siyo kuhusu taifa moja au mawili.”
Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi alisema makubaliano hayo “yanafunga sura yenye maumivu katika historia ya mwanadamu” na kuweka msingi wa suluhisho la mataifa mawili. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Hamas imewaachia huru mateka 20 wa mwisho waliokuwa wamezuiliwa Gaza kwa zaidi ya miaka miwili, huku Israel ikiwaachia wafungwa 1,968 wa Kipalestina. Wakati familia za Waisraeli zilisherehekea kwa machozi ya furaha, maelfu ya Wapalestina walijitokeza Ramallah na Khan Yunis wakipokea wapendwa wao kwa nyimbo na vilio vya shukrani.