Mamia ya mateka wa Kipalestina wameachiliwa huru kutoka jela za Israel siku ya Jumatatu chini ya awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza. Katika uamuzi wa kushangaza jeshi la Israel limetoa onyo dhidi ya kusherehekea hadharani Wapalestina kuachiliwa huru ndugu zao.

Kama sehemu ya makubaliano ya kubadilishana mateka yaliyopatanishwa na pande za kimataifa, Brigedi za al-Qassam – tawi lenye silaha la Hamas – iliwaachilia mateka 20 wa Israel badala ya mateka 1,968 wa Kipalestina, wakiwemo mamia wanaotumikia kifungo cha maisha au kifungo cha muda mrefu.

Hii ni awamu ya kwanza ya mapatano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa kati ya Hamas na utawala ghasibu wa Israel, huku Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) ikiwezesha kukabidhiwa kwa wafungwa na mateka kutoka pande zote mbili.

Wakati huo huo, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imesema kuwa bado ina msimamo wake ule ule wa kuhakikisha mateka wote wa Palestina walioko kwenye makucha ya utawala wa Kizayuni wanaachiliwa huru kutoka kwenye jela za kutisha za Israel.

Suala la kuendelea kukomboa mateka wa Palestina litaendelea kuwa moja ya vipaumbele vyetu vikuu hadi mateka wa mwisho aachiliwe kutoka kwenye jela za Wanazi wapya na kukombolewa maeneo yote ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni ikiwemo Quds Tukufu,” imesema sehemu nyingine ya taarifa ya HAMAS iliyotolewa jana Jumatatu.

Siku ya Ijumaa, makubaliano ya kusitisha mapigano yalifikiwa kati ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS, na hivyo kukomesha miaka miwili ya jinai na mashambulizi ya kigaidi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Ukanda wa Ghaza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *