Wapiganaji wanaodaiwa kuwa na uhusiano na kundi la Dola la Kiislamu (IS) wameua takribani watu 19 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), mamlaka za eneo hilo ziliarifu Jumatatu. Kongo Mashariki, eneo lenye utajiri wa rasilimali na linalopakana na Rwanda, limekumbwa na ghasia kwa zaidi ya miongo mitatu, mara nyingi zikisababishwa na makundi ya waasi wenye silaha.
Kwa mujibu wa maafisa wa jeshi, kundi la Allied Democratic Forces (ADF) — lililoanzishwa na waasi wa zamani wa Uganda na kula kiapo cha utiifu kwa IS — liliwashambulia wakazi wa kijiji cha Mukondo, katika eneo la Lubero, na “kuwaua kikatili watu 19.” Kamanda wa kijeshi wa eneo hilo, Alain Kiwewa, alisema nyumba na maduka yalichomwa moto, na kusababisha wimbi kubwa la wakazi kukimbia makazi yao.
Mamlaka zilipewa tahadhari mapema
Kiongozi wa asasi za kiraia eneo hilo, Kambale Maboko, alisema kati ya waliouawa, 16 ni raia na mmoja ni askari wa Congo, huku wengine kadhaa wakitekwa nyara. Maboko aliongeza kuwa mamlaka zilikuwa zimepewa tahadhari mapema kuhusu uwezekano wa shambulio hilo, lakini “tahadhari hizo hazikuzingatiwa, na matokeo yake ni haya mazito.”
Jeshi la Uganda limekuwa likishirikiana na majeshi ya Congo tangu mwaka 2021 kupambana na ADF, lakini mashambulizi bado yanaendelea. Kundi hilo limekuwa likiwalenga raia wasio na ulinzi kabla ya kujificha kwenye misitu mikubwa ya kanda hiyo. Kwa mujibu wa takwimu za AFP, wapiganaji wa ADF wamewaua zaidi ya watu 180 mashariki mwa DRC tangu mwezi Julai katika mashambulizi kadhaa.