KUNA akili kubwa imechezwa na Yanga kipindi hiki kuna presha kubwa imeelekezwa kwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Romain Folz.
Folz raia wa Ujerumani, amekuwa kwenye presha ya mashabiki wakishinikiza asitishiwe mkataba wake kwa kile wanachokiona Yanga haichezi soka safi licha ya kutopoteza mechi.
Hata hivyo, uongozi wa Yanga ambao awali ulikuwa katika mchakato wa kumuondoa Folz na kumleta Romuald Rakotondrabe ‘Roro’, umesitisha zoezi hilo baada ya kumshusha Patrick Mabedi ambaye ametangazwa kuwa msaidizi wa Folz.
Mabedi ambaye alikuwa Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Malawi, ametua Yanga wakati kikosi hicho kikijiandaa na mechi ya hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Silver Strikers ya Malawi.
Kocha huyo amechukua nafasi ya Manu Rodriguez, aliyekuwa kocha msaidizi kikosini hapo aliyetua sambamba na Folz na ameondoka baada ya kuwasilisha barua ya kuvunja mkataba kutokana na matatizo ya kiafya.
Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti: “Kocha Romain Folz ndiye aliyependekeza jina la Mmalawi huyo ambaye ndiye atakayekuwa msaidizi wake.”

Kutua kwa Mabedi huku Folz akiwa kwenye presha ya kibarua chake sambamba na dili la Roro kuwekwa kando, Mwanaspoti linafahamu lolote linaweza kutokea mbele ya safari kwa Mmalawi huyo kukabidhiwa timu moja kwa moja endapo itahitaji mabadiliko ya benchi la ufundi.
MAMBO MAWILI YA MABEDI
Yanga imemchukua Mabedi kwa sababu kuu mbili ambazo imeziona inaweza kupata faida kupitia kocha huyo, baada ya dili la kocha Roro kuonekana kuingia dosari.
“Kwanza, Yanga imemchukua Mabedi ili kupata ufahamu mkubwa wa wapinzani wetu Silver Strikers tunaokwenda kukutana nao hivi karibuni kwa sababu amewahi kuifundisha timu ya Taifa ya nchi hiyo, hivyo anawafahamu vizuri wachezaji na soka la nchi hiyo.
“Pili, Yanga bado imemweka Folz kwenye mzani na inataka kumwangalia kwenye mechi hizi mbili muhimu, ili kuona matokeo itakayopata ndio yataamua hatma yake, kama ataondoka basi Mabedi ndio atakuwa kocha mkuu kwani ana vigezo vyote vya kusimama kwenye benchi akiwa kocha mkuu.”

MSIKIE MABEDI
Akizungumzia ujio wake Yanga, Mabedi alisema: “Nina furaha kujiunga na timu kama hii kwa sababu vijana hawa wa Jangwani wana mipango mikubwa na mimi ninapenda timu zenye malengo kama hizi.”
Mabedi aliyezaliwa Novemba 5, 1973, kabla ya kuwa kocha, amewahi kucheza soka nafasi ya beki wa kati. Pia amewahi kuitumikia timu hiyo ya taifa ya Malawi akiwa mchezaji na kocha. Anajulikana kwa majina ya utani Bosti au The General.
Katika maisha ya kucheza soka, amepita timu za Big Bullets ya Malawi (1997–1998), Kaizer Chiefs (1998–2006) na Moroka Swallows (2006–2008) zote za Afrika Kusini. Kisha akastaafu kucheza Julai 01, 2008.
Kaizer Chiefs, chini ya kocha Ted Dumitru, Mabedi na Fabian McCarthy waliunda safu imara ya ulinzi iliyoisaidia klabu hiyo kutwaa ubingwa wake wa kwanza wa ligi msimu wa 2003-2004 baada ya miaka 12, kwa mtindo wa kuvutia, wakiwa na tofauti ya pointi sita dhidi ya Ajax Cape Town waliomaliza nafasi ya pili, na wakiwa wamepoteza michezo mitatu pekee msimu mzima.

KAZI YA UKOCHA
Mabedi alianza kazi yake ya ukocha kama mkuu wa kitengo cha vijana cha Moroka Swallows nchini Afrika Kusini kuanzia Septemba 30, 2011 hadi Juni 30, 2015, na baadaye akateuliwa kuwa kocha wa muda timu ya wakubwa msimu wa 2014–2015. Kazi yake ilianza Machi 17, 2015 hadi Machi 25, 2015, kisha alipotua Muhsin Ertugral, yeye akawa msaidizi wake. Nafasi ya kocha msaidizi ndani ya Swallows iliendelea kuanzia Machi 26, 2015 hadi Juni 30, 2015.
Msimu uliofuata, aliondoka Swallows na kujiunga na Mpumalanga Black Aces, ambapo alifanya kazi kama kocha msaidizi wa Ramadhan Nsanzurwimo kuanzia Julai 01, 2015 hadi Agosti 07, 2016. Timu hiyo ilimaliza nafasi ya nne katika Ligi Kuu ya Afrik Kusini, ikiwa pointi 24 nyuma ya mabingwa Mamelodi Sundowns.
Kuanzia Agosti 08, 2016 hadi Septemba 18, 2016, alihudumu kwa muda mfupi kama kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Malawi kabla ya kuteuliwa kuwa kocha mkuu wa Cape Town All Stars, timu aliyoiwezesha kumaliza katika nafasi ya tisa kwenye Ligi Daraja la Kwanza ya Taifa (National First Division) msimu wa 2016–2017. Ilikuwa kuanzia Septemba 19, 2016 hadi Juni 12, 2017.

Mnamo Juni 13, 2017, Mabedi aliteuliwa kuwa kocha msaidizi wa Kaizer Chiefs chini ya Giovanni Solinas. Aprili 23, 2018, alipandishwa cheo na kuwa kocha wa muda (caretaker coach) hadi mwisho wa msimu, Juni 30, 2018.
Julai 01, 2018 hadi Desemba 7, 2018, alikuwa kocha msaidizi wa Kaizer Chiefs chini ya Lionel Soccoia. Wawili hao wakaondoka pamoja na Julai 01, 2019 wakatua Black Leopards, hawakudumu sana, ajira yao ilifika mwisho Septemba 17, 2019.
Kuanzia hapo, akaondoka Afrika Kusini alipodumu kwa muda mrefu na kurejea nchini kwao Malawi, akakabidhiwa kikosi cha timu ya taifa hilo akianza kama kocha wa muda kuanzia Aprili 26, 2023 hadi Oktoba 22, 2023, ndipo akawa kocha mkuu rasmi hadi anatambulishwa ndani ya Yanga. Mkataba wake na Malawi ulikuwa unafikia tamati Desemba 31, 2025.

SIFA ZA UKOCHA
Mabedi alianza kupata Leseni C nchini kwao Malawi, kisha Leseni B na A ya CAF. Akaenda Ujerumani kuongeza ujuzi, akapata Leseni ya UEFA B kisha A kutoka Chama cha Mpira wa Miguu Ujerumani (DEUTSCHER FUSSBALL-BUND).
Sifa hizo zinamfanya kuwa na uwezo wa kukaa katika benchi la ufundi la timu yoyote ya Tanzania inayoshiriki Ligi Kuu Bara kama kocha mkuu kwani amekidhi kigezo cha kanuni ya 77:3 (1,2,3).