Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema usitishaji vita wa Ghaza hautaathiri kesi ya mauaji ya kimbari iliyofunguliwa na nchi yake dhidi ya utawala wa kizayuni wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).

Ramaphosa alitoa kauli hiyo bungeni jana Jumanne mjini Cape Town, akisisitiza kwamba azma ya Afrika Kusini ni kuendeleza kesi yake ya 2023 licha ya makubaliano ya kusitisha vita Ghaza yaliyotekelezwa kupitia mpango unaopigiwa upatu sana na Marekani ukilenga kumaliza vita vilivyoanzishwa na Israel dhidi ya eneo hilo la Palestina lililowekewa mzingiro.

“Mkataba wa amani ambao umeafikiwa, ambao tunaukaribisha, hautakuwa na uhusiano wowote na kesi iliyo mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki,” Ramaphosa ameliambia bunge na kuongezea kwa kusema: “kesi inaendelea, na sasa inatakiwa ifikie kwenye hatua ambapo Israel itapaswa ijibu maombi yetu ambayo yamewasilishwa mahakamani, na wanapaswa kufanya hivyo ifikapo Januari mwaka ujao”.

Afrika Kusini iliwasilisha kesi hiyo Desemba 2023, ikiishutumu Israel kwa vitendo vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Ghaza.

Mnamo Oktoba 2024, Afrika Kusini iliwasilisha mbele ya Mahakama ya Haki ICJ maelezo ya kina la kurasa 500, huku hoja za utawala wa kizayuni za kupinga madai hayo zikitarajiwa kuwasilishwa Januari 12, 2026. Usikilizaji wa kesi unatarajiwa kufanyika mwaka wa 2027, na hukumu ya mwisho inatarajiwa kutolewa mwishoni mwa mwaka huo au mapema 2028.

Nchi kadhaa zimejiunga, au zimetangaza nia ya kufanya hivyo, katika kesi ya ICJ kuiunga mkono Afrika Kusini, ikiwa ni pamoja na Uhispania, Ireland, Uturuki na Colombia…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *