Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu, Abbas Araghchi atazuru Uganda karibuni hivi kushiriki Mkutano wa 19 wa Mawaziri wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM).
Esmaeil Baghaei amesema kaulimbiu kuu ya mkutano huo ni “Kukuza Ushirikiano kwa Ustawi wa Pamoja wa Ulimwengu,”. Ameeleza kuwa, mawaziri wa mambo ya nje na wajumbe wa kidiplomasia kutoka zaidi ya nchi 120 wanachama wa jumuiya hiyo wanatarajiwa kuhudhuria kikao hicho.
Ameongeza kuwa, pamoja na majadiliano ya jumla na kutangaza misimamo ya nchi wanachama, pia kutafanyika kikao cha Kamati ya Palestina ya NAM kwa kushirikisha nchi wanachama wake ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amebainisha kuwa, pamoja na kuwasilisha misimamo ya Iran katika mkutano mkuu wa mawaziri wa mambo ya nje wa NAM, Waziri Araghchi pia atafanya mikutano ya pande mbili na mawaziri wenzake wa nchi mbalimbali pambizoni mwa mkutano huo.
Katika mkutano wa NAM wa mwaka jana huko huko Uganda, pamoja na mambo mengine, Iran ilipendekeza kuitishwa kura ya maoni ili kukidhi matakwa halisi ya mamilioni ya Wapalestina ya kurejea katika ardhi na nchi yao, kwa ajili ya amani ya kudumu huko Palestina.

Weledi wa mambo wanasisitiza kuwa, mpango wa serikali mbili unaoungwa mkono na Marekani na nchi za Magharibi utaandaa mazingira ya kuendelea kujitanua utawala wa Kizayuni.
Haya yanajiri huku utawala wa Kizayuni ukiendelea kukiuka makubaliano ya usitishaji vita Gaza, kwa kuwaua shahidi Wapalestina wa eneo hilo la Palestina.