
Balozi wa Venezuela nchini Iran, José Rafael Silva Aponte amesema Marekani inaihangaisha dunia nzima, ikiwa ni pamoja na Amerika ya Kusini, kwa kutumia kisingizio cha kuleta uhuru katika maeneo tofauti ya dunia, lakini Venezuela daima itasalia kuwa nchi huru na yenye mamlaka ya kujitawala.
Balozi Aponte aliyasema hayo jana Jumanne katika mkutano na waandishi wa habari katika Ubalozi wa Venezuela mjini Tehran, akizungumzia sera za kibeberu za Washington mkabala wa Amerika ya Kusini na eneo la Caribbean, hususan vitisho vyake vya hivi karibuni vya kijeshi dhidi ya Venezuela.
Ameashiria nukuu maarufu ya Simón Bolívar, mwanasiasa na kiongozi wa kijeshi wa Venezuela ambaye aliongoza mapinduzi yaliyopelekea Colombia, Venezuela, Ecuador, Peru, Panama, na Bolivia kupata uhuru kutoka kwa utawala wa Uhispania kati ya 1819 na 1825.
Bolívar aliandika katika barua kwamba, “Marekani inaonekana kuwa imekusudiwa na Providence kulibughudhi eneo la Amerika kwa taabu kwa kisingizio cha uhuru,” Balozi huyo alisema, akiongeza kuwa mwenendo huu leo hii si unaelekezwa kwa Venezuela, lakini unaenezwa kote ulimwenguni.
Ameongeza kuwa, Washington pia inaeneza simulizi za uwongo zinazomtuhumu Rais Nicolás Maduro kwa kuhusika na ulanguzi wa dawa za kulevya, kwa lengo la kusimika “vibaraka” wake madarakani. Balozi wa Venezuela hapa Tehran amebainisha kuwa, lawama hizo hazina msingi, hasa ikizingatiwa kuwa nchi nyingine kama vile Colombia na Ecuador zinahusika zaidi na ulanguzi wa dawa za kulevya, na kwamba ni asilimia 5 tu ya mihadarati hupitia Venezuela.
Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, ameonya kuwa shambulio lolote dhidi ya taifa lake kwa kisingizio chochote litakabiliwa kwa mshikamano wa mataifa ya ukanda huo, akisisitiza kuwa nchi hiyo katu haiwezi kuwa koloni la Marekani wala kutawaliwa na maajinabi.