Singida. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimewaahidi wananchi wa Mkoa wa Singida ujenzi wa kiwanda cha mafuta ya alizeti ili kuchochea shughuli za kilimo na ajira.

Ahadi hizo zimetolewa leo Jumatano, Oktoba 15, 2025 na mgombea mwenza wa urais wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi katika mikutano ya kampeni mkoani Singida.

Mkutano wa kwanza umefanyikia eneo la Puma, ikihusisha majimbo ya Ikungi Magharibi na Ikungi Mashariki na wa pili, umefanyikia Uwanja wa Mitundu, ukihusisha Jimbo la Itigi na Manyoni.

Dk Nchimbi amesema wananchi wa Singida wanajishughulisha na kilimo na alizeti ni miongoni mwao na endapo wakishinda uchaguzi wanakwenda kujenga kiwanda mkoani humo.

“Tumesema Singida ina haki ya kuwa na viwanda, Ikungi nayo ina haki ya kuwa na viwanda na maeneo yatakayozingatiwa ni pamoja na viwanda vya mafuta ya alizeti ili kuwasaidia wakulima, kuongeza ajira, na kupunguza uagizaji wa mafuta ya kupikia kutoka nje,” amesema Dk Nchimbi.

Tanzania inaendelea kuagiza kiwango kikubwa cha mafuta ya kupikia nje ya nchi licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa ndani, hasa kupitia kilimo cha alizeti.

Mkoa wa Singida ni miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa uzalishaji wa alizeti nchini hivyo kuufanya kuwa eneo bora kwa uwekezaji wa viwanda katika sekta hiyo, vikihusisha utengenezaji wa chakula cha mifugo kwa kutumia mabaki ya alizeti, hatua inayolenga kuunga mkono sekta ya mifugo na kuimarisha usalama wa chakula.

Ahadi hiyo inaendana na ilani ya uchaguzi ya CCM, ambayo inatamka wazi nia ya kuanzisha viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo, nyama na maziwa kama sehemu ya mkakati wa kuinua uchumi wa vijijini na kupanua fursa za ajira.

“Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali ya CCM inalenga kutengeneza ajira milioni nane kwa vijana. Maendeleo ya viwanda, hasa katika uchakataji wa mazao ya kilimo na mifugo, yatakuwa kiini cha mafanikio haya,” amesema Dk Nchimbi.

Amesema mambo muhimu yatakayowezesha maendeleo hayo ya viwanda ni pamoja na upatikanaji wa mbolea na mbegu bora kupitia ruzuku itakayoongeza na kufikishwa kwa wakilima kwa wakati.

Baadhi ya barabara ambazo zitajengwa ni ya Itigi Mjini kwa kiwango cha lami, ukamilishaji wa ujenzi wa barabara ya Sabasaba Sepuka Ndago Kiswaga kilomita 74,   ujenzi wa barabara ya Ikungi Londoni hadi Solwa kilomita 117.

Amesema ujenzi wa barabara ya Singida, Magereza Tunduru kwa kiwango cha lami kilomita 113, ujenzi wa barabara ya Puma Ihanja Mshiti. Ujenzi wa barabara ya Handeni Kiberashi Kibaya, Njoro Goima Tambalale Chemba Kwamtoro mpaka Singida kilometa 498.

Mbali na ahadi hizo, Dk Nchimbi akiwa Ikungi na Manyoni ameahidi ujenzi wa shule za msingi na sekondari, kuboresha sekta ya afya kwa kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kujenga zahanati na vituo vya afya.

Pia, kuongeza upatikanaji wa maji kwa kuanzia miradi mikubwa ili kuwapunguzia adha wananchi.

“Ninawaomba, tujitokeze kuipigia kura CCM, tumchague mama Samia, wabunge na madiwani wetu ili tukachape kazi,” amesema Dk Nchimbi.

Awali, mgombea ubunge wa Ikungi Magharibi, Elibariki Kingu amesema mambo mengi yamefanyika jimboni humo na kumweleza Dk Nchimbi kwamba wataongoza kwa kura za Rais katika uchaguzi huu ujao

Kingu amesema hakuna kata katika jimbo hilo ambapo imeachwa, miradi imepelekwa na Serikali ya Rais Samia na kumweleza Dk Nchimbi asiwe na wasiwasi kwani ushindi upo ikiwemo kwake yeye mwenyewe ili aendelee kuwawakilisha bungeni wananchi.

Mgombea ubunge wa Itigi, Msita Stephen amesema jimbo hilo lina kata 13 na kati ya hizo, kata tatu zina vituo vya afya, miradi ya maji imetekelezwa.

“Rais Samia ametugusa katika kila eneo, kituo kizuri cha afya Itigi kimejengwa, Hospitali ya Wilaya imejengwa ingawa Itigi bado haijawa wilaya, maji yanatoka maeneo mengi, shule zimejengwa,” amesema.

Stephen amesema wananchi wanaomba kutengenewa barabara ya lami kutoka Itigi hadi Rungwa. Pia, mpaka wa Pori la Akiba lisogezwe ili kuwapa wananchi wa Itigi hususan wa Mitundu wapate eneo la makazi na uchimbaji.

Amesema kumekuwa na ucheleweshaji wa malipo ya tumbaku: “Na tangu mazao yao yamechukuliwa, wanadai fedha nyingi, tunaomba mgombea mwenza utusaidie kwa hili.”

Alichokisema Dk Mwigulu

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ambaye pia ni mgombea ubunge wa Iramba Magharibi, Dk Mwigulu Nchemba akiwa Itigi amesema shughuli ya kupiga kura ni ya wote: “Hakuna kutuma mwakilishi. Hata kama unakwenda kuchunga, siku hiyo twendeni kupiga kura kwanza ndiyo uende kuchunga.”

Dk Mwigulu ambaye ni Waziri wa Fedha amesema: “Mimi ni msaidizi wa Rais Samia, nina ushahidi wa kilichofanyika, tunakwenda kupiga kura kwa sababu tunaowachagua tuna uhakika nao. Tunakwenda kupiga kura kwa sababu tuna mambo tunayasubiri kama barabara ya lami, mpaka usogee na mengine mengi.”

Dk Mwigulu amesema amekua serikalini tangu awamu ya nne, ya tano na sasa ya sita: “Hakuna awamu imepeleka fedha za miradi ya maendeleo kama hii, sasa nawaomba msisikilize maneno ya watu, twendeni kupiga kura.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *