Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kundi la waasi la M23 wametia saini makubaliano mjini Doha ya kuanzisha utaratibu wa ufuatiliaji na uhakiki wa usitishaji mapigano, chini ya upatanishi wa Qatar.

Utiaji saini huo wa jana, ambao umekuja mwezi mmoja baada ya kuundwa kwa utaratibu wa kubadilishana na kuachiliwa kwa wafungwa, unaashiria “hatua kubwa” katika kutekeleza Azimio la Kanuni lililotiwa saini na Kinshasa na M23 mwezi Julai, kwa mujibu wa taarifa ya serikali ya DRC.

DRC imesisitiza kujitolea kwake kufikia usitishaji wa uhasama, kuhakikisha usalama wa raia, na kuweka msingi wa makubaliano ya amani ya kina na ya kudumu ndani ya Mchakato wa Doha unaoungwa mkono na jamii ya kimataifa.

“Hii ni hatua muhimu kwenda mbele,” Msemaji wa M23, Lawrence Kanyuka amesema kwenye mtandao wa kijamii wa X, akitoa radimali yake kuhusu kutiwa saini kwa utaratibu huo.

Makubaliano ya amani yaliyopendekezwa kati ya serikali ya DRC na waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda yanataka kurejesha udhibiti wa serikali katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi.

Serikali ya Kongo DR na waasi wa M23 kila upande unautuhumu upande wa pili kuwa umekiuka makubaliano ya kusitisha vita. 

Mapigano kati ya wanajeshi wa serikali na waasi wa M23 yaliongezeka mwezi Januari, wakati waasi hao walipoteka sehemu kubwa ya mashariki yenye utajiri wa madini, ukiwemo mji wa Goma.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, maelfu ya watu wameuawa na mamia kwa maelfu ya raia kulazimishwa kuyaacha makazi yao kutokana na vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *