
Watumiaji wa mitandao ya kijamii wameikosoa vikali serikali ya India kwa kuendelea kuwatia mbaroni na kuwashtaki Waislamu wanaoendeleza kampeni ya nchi nzima ya ‘Nampenda Muhammad’.
Katika muda wa mwezi mmoja uliopita, polisi wa India wamevamia masoko na nyumba nyingi, wakiwakamata wanaume Waislamu katika majimbo yanayoongozwa na chama tawala cha Waziri Mkuu, Narendra Modi kwa kubeba mabango yanayosema ‘Nampenda Muhammad’.
Wamekamatwa tu kwa kuandika, “Nampenda Muhammad” kwenye mabango, fulana, au katika jumbe za mitandao ya kijamii. Mamlaka ya India inadai kuwa usemi huo eti unatishia “nidhamu ya umma”.
Hadi sasa, takriban kesi 22 zimesajiliwa dhidi ya Waislamu zaidi ya 2,500. Takriban watu 40 wamekamatwa katika majimbo mengi yanayosimamiwa na chama cha Bharatiya Janata Party (BJP), kwa mujibu wa Shirika la Kulinda Haki za Kiraia (APCR).
Aidha makumi ya Waislamu wamekamatwa katika majimbo tofauti – wakiwemo baadhi katika jimbo la Gujarat, nyumbani kwa Modi- kwa kutuma jumbe za mitandao ya kijamii na video zilizo na maneno “Nampenda Muhammad”.
Waislamu wa India, ambao ni zaidi ya watu milioni 200, katika miaka ya hivi karibuni wamekuwa wakikabiliwa na changamoto zinazoongezeka katika uwanja wa haki za uraia, usalama wa kijamii na ushiriki wa kisiasa.
Tangu iingie madarakani mwaka 2014, serikali ya Narendra Modi, Waziri Mkuu wa India na kiongozi wa chama cha BJP imetekeleza sera ambazo zinaelezwa na wadadisi wengi wa ndani na kimataifa kuwa ni mfululizo wa hatua za ubaguzi, upendeleo na chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.