
Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama ya Jihadul Islami ya Palestina amepuuzilia mbali wazo la kupokonywa silaha wanamuqawama na kusema kuwa, makundi ya mapambano ya Kiislamu ya Palestina hayajaafiki kipengele kinachohusiana na upokonyaji silaha.
Kanali ya Al-Jazeera imemnukuu Mohammad Al-Hindi akisema hayo na kuongeza kuwa, mrengo wa Muqawama hautakubali vitisho vya kupokonywa silaha zao kwa nguvu.
Amefafanua kuwa, hakuna vipengee vya siri katika makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza, na kuongeza kuwa madai yanayosambazwa na utawala wa Israel ni “uvumi tu usio na ukweli wowote.”
Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Jihadul Islami ameongeza kuwa, kuna uwezekano wa utawala wa Kizayuni kukwamisha utekelezaji wa makubaliano hayo ya kusitisha mapigano Gaza.
Mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yaliyofanyika nchini Misri kati ya Israel na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS yaliipelekea kufikiwa makubaliano ya kusimamisha vita Gaza, kuondoka wanajeshi vamizi wa utawala wa Kizayuni kwenye ukanda huo na kubadilishana mateka.
Al-Hindi amesisitiza kuwa, mirengo ya Muqawama inafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mapatano hayo ili kuhakikisha kuwa haki za watu wa Palestina zinadumishwa.
Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina imepongeza kuachiliwa huru mateka wa Palestina katika jela za kuogofya za kutokana na ushujaa wa wamamapambano wa kambi ya Muqawama na nguvu za mshikamano na umoja wa kitaifa wa Wapalestina.