Dar es Salaam. Unamkumbuka lejendari wa Bongofleva, Juma Kassim Kiroboto? Mwamba wa muziki wa kizazi kipya aliyeibuka na kupata umaarufu akitumia jina la Juma Nature? Mkali huyo na mmoja wa wanamuziki wa mwanzo kabisa kufanya mapinduzi makubwa katika muziki huo miaka ile ya mwishoni mwa tisini na mwanzoni mwa elfu mbili ana mengi kwa wasanii wanaochipukia.

Nature ambaye ni miongoni mwa waanzilishi wa lile kundi maarufu la muziki la TMK Wanaume Family lililoundwa na wakali wa kuchana kutoka mitaa ya Temeke, Dar es Salaam, amepiga stori na Mwananchi, lakini katika mengi amedondosha ushauri kwa serikali akiiomba kuanza kuchuja baadhi ya nyimbo ambazo zinaleta ukengeufu kwa watoto ambao wanapaswa kujengwa katika misingi ya maadili, imani na kuwapa elimu sahihi.

“Nafahamu kwa dunia ya leo ni ngumu sana (kudhibiti), ila serikali ikidhibiti basi yapo mambo yatapungua. Unakuta nyimbo za kupigwa baa ama klabu zinapigwa na bodaboda au majumbani ambako kuna watoto ambao ndio wanazishika zaidi na kuanza kuimba,” anasema Nature.

“Kuwasomesha watoto na kufanya wazungumze Kiingereza hilo pekee halitoshi, bali tunatakiwa kuwapa vitu vyema kwa sababu  hao ndio viongozi wetu wajao. Je tumewahi kufikiria wakikua watakuwa watu wa aina gani endapo hakutakuwa na mabadiliko ya kulinda desturi zetu kama ilivyo sasa?”

NATU 01

Kwa mwanamuziki huyo jambo jingine kubwa ni kwa wasanii chipukizi kuandika mashairi yenye maadili kwa jamii  yatakayozingatia kujenga kizazi chenye nguvu na viongozi mahiri katika ngazi mbalimbali nchini.

Nature anasema kuna haja kwa wasanii wanapotunga nyimbo wasiwe na haraka ya kuzitoa kwa jamii na kwenda na upepo wa kuzungumziwa wakati zikiwa hazina ujumbe wa maana, bali unaobomoa.

“Kuna aina mbili ya muziki, wapo wenye vipaji vya kuzaliwa na kujifunza wote hao wanapaswa kujua kitu gani wanapaswa kukifanya katika jamii na isiwe ilimradi wanasikika katika vyombo vya habari,” anasema na kuongeza:

“Mfano kuna nyimbo zinatakiwa zipigwe klabu ama usiku kwa kuzingatia rika ambazo zinaweza zikawa zinazungumzia vitu vikubwa ambavyo havihusiani na watoto wadogo ambao wanapaswa akilini mwao kuingiza vitu vinavyowafaa.

“Ajabu kuna nyimbo zinazopigwa mtaani ambazo zingine zimejaa matusi ndani yake. Unakuta mtoto ana umri wa miaka mitano anaimba nyimbo ambayo ukisikiliza mtu mzima unaona aibu. Wengine tumeshakuwa watu wazima tunaitwa babu, hivyo hatuoni kama hilo linajenga.”

NATU 02

Nature anamtolea mfano lejendari wa muziki wa reggae, Bob Marley ambaye licha ya kufa miaka mingi iliyopita, lakini ujumbe wa nyimbo zake umebaki katika jamii duniani kote jambo linaloonyesha kwamba alitumia akili kuandika mashairi yanayoishi.

“Ukisikiliza muziki wa Bob Marley utahisi ameimba jana, mfano ‘No woman, No Cry’, ‘Get Up Stand Up’, ‘One Love’ zote hizi zikipigwa zinaleta kitu cha tofauti katika hisia za watu. Hilo ni funzo linaloonyesha maana halisi ya watu maarufu kuwa kioo cha jamii,” anasema mkongwe huyo.

“Wasanii wajifunze kuacha alama kwa watu, lakini wakipenda kutrendi peke yake baadaye wakija kupotea watakuwa wamepoteza nguvu zao na hazitathaminiwa.”

Anasema watu maarufu ni pamoja na wanasoka akimtolea mfano staa wa zamani wa Manchester United, Real Madrid, Juventus na Al-Nassr, Cristiano Ronaldo ambavyo anazungumziwa na jamii kutokana na kile anachofanya ndani na nje ya uwanja.

NATU 03

“Ronaldo amekuwa mfano wa kuigwa kwa namna ambavyo anaheshimu misingi ya kazi na anavyojitoa kwa jamii hilo litabaki kusimuliwa na mashabiki hata kama ataacha soka, hivyo lazima kila mtu maarufu ajue kile anachofanya (kuwa) wapo wanaokichukua kama kilivyo,” anasema Nature aliyefanya muziki zaidi ya miaka 25.

Msanii huyo anasema katika kuhakikisha maisha yake na jamii inayomfuatilia hayaathiri na mtindo mchafu unaotumiwa na baadhi ya watu kutrendi, amekuwa haendeshwi na mitandao ya kijamii na badala yake yeye ndiye anayeiendesha kwani kile alichofanya katika muziki kinamwezesha kila kitu akifanye kwa usahihi.

NATU 04

“Kazi nilizozifanya zinatosha kunitambulisha katika mitandao ya kijamii ndiyo maana huwezi kuona napenda mambo ya kiki. Hata wasanii wa sasa kama wanafanya hizo kiki, basi muziki wao uwe mzuri na siyo matukio feki yawe makubwa kuliko uhalisia wa kile wanachokitoa kwa jamii,” anasema.

Jambo lingine analolisisitiza ni wasanii kujitahidi kuwa wabunifu huku wakiacha mambo ya kuigana

“Mfano muziki wa singeli mmoja akiimba mama Amina kila mtu lazima aliweke hilo jina. Waache uvivu wazifikirishe akili zao.”

Nature anasema katika albamu yake ya kwanza kuna wimbo unaitwa Chanzo Nini ambao anaamini watu wakiusikiliza watajifunza mambo fulani hasa kwa wasanii kujitahidi kuandika mashairi yanayobeba uhalisia wa maisha ya jamii.

“Nina albamu tano, lakini kuna wimbo unaitwa Chanzo Nini ukiusikiliza utanielewa, kwani bado una nguvu na ujumbe muhimu kwa taifa,” anasema Nature anayemtaja kipa wa zamani wa Simba na Yanga, Juma Kaseja kuwa miongoni mwa wanasoka aliokuwa anawakubali enzi hizo wakicheza.

NATU 05

Kwa vijana wa sasa wasiomjua vyema mwanamuziki huyo na hasa maana ya jina la Nature analolitumia kama a.k.a mkongwe huyo anasema wakati anaamua kulitumia aliamini kwamba linamfaa kutokana na aina ya maisha anayopenda kuishi kuwa ni yale halisi na si kufeki kama baadhi ya wasanii na watu maarufu wanavyopenda kufanya.

“Nature sijapewa na raia, bali nilisoma nikaelewa lina maana ya ‘halisi’ na mimi maisha yangu ni halisi. Hivyo nikaona linaendana na nilivyo, kwa kifupi ni hivyo,” anasema.

“Jina la Sir nilijipa mimi mwenyewe pia baada ya kusoma mambo ya skauti ambapo niliona mwanzilishi alikuwa anaitwa Sir Robert Stephanson Symith Baden Powell ndipo na mimi nikajiita Sir.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *