Leo ni Jumatano mwezi 22 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1447 Hijria mwafaka na tarehe 15 Oktoba 2025 Milaadia
Siku kama ya leo miaka 1151 iliyopita, kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Musa al-Mubarqa’ mtoto wa Imam Muhammad Taqi al-Jawad na ndugu wa Imam Hadi AS aliaga dunia katika mji mtakatifu wa Qum, Iran. Alizaliwa Madina mwaka 214 Hijria na mpaka anafikisha umri wa miaka 6 ambapo baba yake aliuawa shahidi, alikuwa chini ya malezi na usimamizi wa baba yake huyo. Baadaye alijifunza elimu kwa kaka yake, yaani Imam al Hadi AS. Musa al-Mubarqa’ kipindi fulani aliishi katika mji wa Kufa katika Iraq ya leo na alipokuwa na umri wa miaka 42 alisafiri na kuelekea katika mji wa Qum, Iran. Aliishi Qum akijishughulisha na ulinganiaji na kueneza dini ya Uislamu hadi alipofariki dunia katika siku kama ya leo. Musa al-Mubarqa’ ana daraja ya juu ya kielimu na alikuwa mpokezi wa Hadithi. Aidha alisifika mno kwa taqwa na uchamungu.***

Siku kama ya leo miaka 483 iliyopita alizaliwa Abul-Fat’h Jalal al-Din Muhammad Akbar, mfalme aliyekuwa na nguvu kubwa wa silsila ya Teimurian nchini India. Mfalme huyo alikuwa maarufu kwa jina la Akbar Shah na alichukua madaraka akiwa na umri wa miaka 13 baada ya kufariki dunia baba yake, yaani Homayun. Kwa kipindi cha miaka mitano aliongoza nchi akiwa na cheo cha naibu mtawala chini ya usimamizi wa Bairam Khan. Baada ya kushika madaraka kikamilifu alianza kupanua wigo wa utawala wake katika maeneo ya Bengal, Kashmir, Sindh, Punjab, Ahmednagar na Kandahar. Mfalme Abul-Fat’h Jalal al-Din Muhammad Akbar alikomboa kisiwa cha Dakan huko kusini mwa India kutoka mikononi mwa Wareno. Akbar Shah alifariki dunia mwaka 1605.

Katika siku kama ya leo miaka 185 iliyopita, alizaliwa mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Muhammad Taqi Razi, katika mji wa Isfahan nchini Iran. Sheikh Taqi Razi maarufu kwa jila la Agha Najafi, alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq kwa ajili ya elimu ya juu ya kidini baada ya kukamilisha elimu ya msingi. Alipata elimu kwa wanazuoni mashuhuri kama Mirza Muhammad Hassan Shirazi na Sheikh Mahdi Kashiful Ghitaa. Baada ya kurejea Isfahan, Sheikh Agha Najafi alikuwa marejeo ya Waislamu katika masuala ya kidini na kisheria. Alikuwa mstari wa mbele kupambana na wakoloni kupitia harakati iliyopewa jina la Harakati ya Tumbaku. Vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni pamoja na “Anwarul Arifin”, “Asrarul Ayat” na “Al-Ijtihad Wattaqlid”. ***

Siku kama ya leo miaka 181 iliyopita alizaliwa mwanafalsafa wa Kijerumani Friedrich Wilhelm Nietzsche. Baada ya kuhitimu masomo, Nietzsche alianza kufunza katika Chuo Kikuu cha Basel. Mwanafalsafa huyo alikuwa akipinga dini na misingi ya kimaadili na katika falsafa na mitazamo yake alikuwa akiamini nadharia ya “Superman”, kwa maana ya mtu mwenye uwezo kupita kiasi. Nietzsche alikuwa akiamini kwamba, mtu mwenye uwezo kupita kiasi au Superman ni matokeo ya irada na matashi ya mwanadamu na huwa juu ya mema na mabaya yote. Mwanafalsafa huyo ameandika vitabu kadhaa ikiwa ni pamoja na Beyond Good and Evil, The Birth of Tragedy na Thus Spoke Zarathustra. Katika kipindi cha mwishoni mwa uhai wake Friedrich Wilhelm Nietzsche alipoteza mlingano wa kifikra na alifariki dunia mwaka 1900. ***

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya kiirani, yaani tarehe 23 Mehr 1361 Hijria Shamsia, Ayatullah “Ata’ullah Ashrafi Isfahani”, mwakilishi wa Imam Khomeini (RA) na Imam wa Sala ya Ijumaa ya Kermanshah – moja ya miji ya magharibi mwa Iran – aliuawa shahidi katika mihrabu ya ndani ya Msikiti na maajenti wa genge la kigaidi la Wanafiki, MKO. Wakati wa mapambano yaliyopelekea kupatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Ayatullah Ashrafi Isfahani aliwaongoza wananchi wa Kermanshah katika mapambano dhidi ya utawala wa Shah na ndio maana alikamatwa na kutiwa gerezani mara nyingi. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, mwanazuoni huyo mkubwa aliteuliwa kuwa Imam wa Sala ya Ijumaa ya Kermanshah kwa amri ya Imam Khomeini (RA) na tarehe kama hii ya leo, wakati alipokuwa akisalisha Sala ya Ijumaa, maadui wa Uislamu walimuua shahidi kwenye Mihrabu ya Sala. Baada ya kuuawa shahidi Ayatullah Ashrafi Isfahani, Imam Khomeini (RA) alisema: “Nilikuwa namfahamu marhum, shahidi mtukufu Hajj Agha Ata’ullah Ashrafi kwa muda mrefu kwa usafi wake wa nafsi, utulivu wa akili na moyo wake usiotetereka. Aliyepambana vilivyo na hawaa na matamanio ya nafsi na alipambika kwa ilmu na maarifa mengi yenye manufaa na matendo mema. ***

Na leo tarehe 15 Oktoba ni Siku ya Vipofu Duniani. Suala la usalama wa vipofu na haki zao za kijamii daima lilikuwa likipewa umuhimu maalumu katika jumuiya za kimataifa na kwa msingi huo mwaka 1950 Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) na Baraza la Kimataifa la Vipofu zilikutana na kupasisha sheria ya Fimbo Nyeupe na kuitangaza tarehe 15 Oktoba kuwa ni Siku ya Fimbo Nyeupe au Siku ya Kimataifa ya Usalama wa Vipovu. Miongoni mwa vipengee vya sheria hiyo ni pamoja na haki ya vipofu kutumia suhula zote za hali bora ya kimaisha katika jamii, kuwahamasisha watu wa jamii hiyo kushiriki katika masuala ya serikali na kupewa ajira serikalini, kulinda haki za vipofu wakati wa kuvuka barabara na kadhalika. ***
