
Viongozi mbalimbali duniani, wamekuwa wakitoa salamu zao za pole kwa wananchi wa Kenya, kufuatia kifo cha Raila Odinga.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, amesema amesikitishwa na rafiki yake Raila Odinga na kumkumbuka kama rafiki wa karibu wa India.
Rais mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta, amemkumbuka Raila kama mtoto wa kweli wa Kenya, aliyeipenda nchi yake. Uhuru ameongeza kuwa, amehunika kumpoteza rafiki na kaka yake.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mheshimiwa Raila Amolo Odinga, aliyemtaja kiongozi mahiri, Mwanamajumui wa Afrika, mpenda amani na mtafuta suluhu, ambaye ushawishi na upendo wake haukuwa tu ndani ya Kenya, bali Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.
Nacho chama cha cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA nchini Tanzania, nacho kimesema Odinga atakumbukwa kama mwanasiasa mzalendo na shujaa wa dempkrasia aliyejitolea kupigania haki, ujumbe uliotolewa pia na kiongozi wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine.
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, rais wa Djibouti Ismail Omar Guelleh, na rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa wamesema Kenya imempoteza kiongozi mwenye maono, ujumbe ambao pia umetolewa na rais wa Zambia Hakainde Hichilema.
Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia Katibu Mkuu wake Veronica Nduva, pia ametoa ujumbe kama huo na kusema Kenya imempoteza kiongozi shupavu.
Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Mahmoud Ali Youssouf, amemwomboleza Raila kama kiongozi shupavu wa Afrika, aliyetoa mchango mkubwa ndani na nje ya Afrika.