
Kenya imekumbwa na msiba mzito, kufuatia kifo cha kiongozi mashuhuru wa upinzani na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, aliyefariki dunia Jumatano asubuhi akiwa na umri 80 baada kupata mshtuko wa moyo, wakati akipokea matibabu nchini India.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Raila Odinga, alizaliwa Januari 7 mwaka 1945, Magharibi mwa Kenya, baba yake Jaramogi Oginga Odinga, alikuwa Makamu wa Kwanza wa rais wa Kenya, baada ya kupata uhuru.
Odinga, ambaye alipewa majina mengi kutokana na umahiri wake wa siasa za upinzani, kama Baba, Agwambo, Tinga na mengine, katika maisha yake yote amehusika pakubwa kwenye siasa za Kenya.
Mpigania demokrasia, ujio wa vyama vingi, na haki za wananchi wa kawaida, Raila Odinga alifungwa jela miaka nane, kipindi cha uongozi wa aliyekuwa rais Daniel Arap Moi, kutokana na harakati zake za kisiasa.
Aliingia bungeni kwa mara ya Kwanza mwaka 1992, akiwalisha eneo Bunge la Langa’ta jijini Nairobi.
Baadaye, tangu mwaka 1997, alianza kujitosa kwenye kinyanganyiro cha urais, wadhifa alioutafuta mara tano, mwaka 2007, 2013, 2017 na 2022, lakini hakufanikiwa kuingia Ikulu, kwa nyakati hizo zote, kulikuwa na madai makubwa ya kuibiwa kura.
Aliposhiriki uchaguzi wa mwaka 2007, nchi iliingia kwenye machafuko makubwa ya kisiasa, baada ya chama chake cha ODM kudai kuibiwa kura na kuishia kuundwa kwa serikali ya muungano ambao alishika wadhifa wa Waziri Mkuu kati ya mwaka 2007 hadi 2013.
Mwezi Februari mwaka huu, Odinga alijitosa kwenye nafasi ya kutafuta Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika lakini hakupa nafasi hiyo. Mwaka 2024 aliingia kwenye mkataba wa kisiasa na rais William Ruto na kuingia serikalini.
Kiongozi huyo wa chama cha ODM, atakumbukwa kama mpenda maridhiano ya kisiasa, mwanamajumui wa Afrika na mpenda Jumuiya ya Afrika Mashariki.