
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov amesema kivuli cha ukoloni kinasalia kuwa chanzo kikuu cha migogoro barani Afrika, na wakoloni wa zamani, sasa hivi wanajaribu kukwepa uwajibikaji kwa kuilaumu Moscow.
Lavrov amesema hayo katika mahojiano ambapo ameshutumu madola ya Magharibi kwa kupanda kwa makusudi mbegu za migawanyiko katika bara zima la Afrika.
“Wakoloni walichora mistari iliyonyooka kote barani Afrika, wakigawanya maeneo na kuyaweka katika mapote ya kikabila,” Lavrov ameelezea.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Russia amekanusha madai kwamba jeshi la Russia linaiyumbisha Afrika kupitia operesheni zake za kijeshi.
Amefafanua kuwa, kuongeza uwepo wake barani humo, kunatokana na mataifa kadhaa yakiwemo Afrika Kusini, Niger na Burkina Faso kuiangalia Russia kama mshirika wa kuaminika.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema Moscow imebaki kuwa mshirika wa kweli na wa kuaminika kwa mataifa ya Afrika kwa kusaidia juhudi za kuimarisha mamlaka zao, ambazo zinatishiwa na aina za kisasa za ukoloni kupitia njia mbali mbali kama magenge ya kigaidi.
Ameashiria msaada wa muda mrefu wa Russia kwa mataifa ya Afrika, ulioanza enzi za Umoja wa Kisovyeti (USSR) ambapo Moscow iliunga mkono harakati za ukombozi wa kitaifa na kusaidia katika kuangusha mifumo ya kikoloni.
Moscow imetangaza kuwa, kukuza mahusiano na mataifa ya Afrika ni miongoni mwa vipaumbele vyake vikuu vya sera za nje.